SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) wamewatembelea wajasiriamali kujua changamoto zao sambamba na kuwapa elimu ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao katika Maonesho ya 30 ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yanayofanyika kwenye viwanja vya Nanenane Themi- Njiro Jijini Arusha.
Akizungumza katika Maonesho hayo leo Agosti 5, 2024, Afisa udhibiti Ubora wa TBS, Bw. Abdallah Mkanza amesema Serikali inatenga kati ya 150M -200M kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo mbapo mpaka sasa zaidi ya wajasiriamali wadogo 1500 kutoka mikoa mbalimbali wamepata leseni chini ya mpango huu wa bure.
Aidha, amesema kupitia maonesho hayo pia wanatoa msaada kwa wateja kwenye huduma mbalimbali za Shirika kama usajili wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi , leseni ya kutumia alama ya ubora na msaada wa kitaalam kwa wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi pamoja na umuhimu wa kusoma taarifa za kwenye vifungashio hususani muda wa mwisho wa matumizi ( expire dates).
Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Masoko TBS, Bi. Gladness Kaseka ametoa wito kwa wateja na wananchi kutumia fursa hiyo kwa kutembelea banda la TBS lililopo ndani ya viwanja hivyo na watakaoshindwa wasisite kuwasiliana na TBS kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa namba ya bure 0800110827.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu "Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo,mifugo na uvuvi", yameanza rasmi tar 01/08/2024 na kufunguliwa rasmi tarehe 03/08/2024 na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe.Nurdin Babu
Social Plugin