NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limefungua mashindano ya tuzo za ubora kitaifa awamu ya tano kwa mwaka 2024/2025 ili kuweza kuwatambua na kuwapongeza watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu ya ubora au taasisi zinazofanya vizuri kwenye masuala ya ubora wakati wa utekeleza wa shughuli zao za utoaji huduma.
Akizungumza wakati akifungua mashindano hayo leo Agosti 14,2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amesema mashindano hayo yatahamasisha ubunifu na uboreshaji wa bidhaa na huduma zinazotolewa nchini kupitia taratibu zilizowekwa chini ya miundombinu ya ubora.
Aidha amesema tuzo za ubora kwa awamu ya tano kwa mwaka 2024 zimeandaliwa kwenye vipengele vitano ambavyo ni kipengele cha cha tuzo kwa kampuni bora ya mwaka, tuzo kwa bidhaa bora ya mwaka, tuzo kwa huduma bora ya mwaka, tuzo kwa muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na kipengele cha tano ni tuzo kwa mtu mmoja aliyefanya vizuri kwenye masuala ya ubora na washindi watashiriki katika ngazi ya EAC pamoja na SADC
Amongeza kuwa washindi wa tuzo za kitaifa awamu ya nne kwa mwaka 2023/2024 walishiriki katika mashindano ya tuzo za ubora kwa nchi za SADC ambapo washiriki wa Tanzania walifanikiwa kupata ushindi katika vipengele vitatu.
"Washiriki wa Tanzania walifanikiwa kwenye mshindi wa pili wa SADC tuzo ya muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi (East Cost Oil and Fats Ltd), mshindi wa tatu kampuni ya bora ya mwaka ya SADC (Mjasiriamali)- CAPS Tanzania Ltd, mshindi wa tatu mota huduma bora wa SADC (Mjasiriamali)- CAPS Tanzania Ltd". Amesema Dkt. Katunzi.
Pamoja na hayo amesema kipengele cha kwanza hadi cha nne wameandaa tuzo kwenye makundi mawili kwa kila kipengele ambapo tuzo kwa kampuni kubwa na pia tuzo kwa kampuni ndogo au wajasiriamali wadogo. Na kipengele cha tano kinahusisha tuzo moja kwa mtu mmoja pekee
Hata hivyo amesema maandalizi, usimamizi na tathimini ya tuzo hizi yanafanywa na kamati maalum ambayo inahusisha taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara, TPSF, TBS, ZBS, TCCIA, SIDO, ZEEA, ZNCCA, TWCC, NQAT, TANTRADE pamoja na taasisi nyingine.
Ameeleza kuwa miongoni mwa vigezo vinavyotumika kuwapata washindi ni pamoja na nini kinafanywa na taasisi husika au mtu binafsi kuoneza ubora wa bidhaa, huduma, ufanisi katika uzalishaji au utendaji kazi kwa ujumla.
Amesema kigezo kingine ni pamoja na ni kiasi gani taasisi au mtu binafsi ameweza kunufaika kwa kuongeza ubora wa bidhaa, huduma au utendaji kazi na vilevile ni kwa namna gani biashara imekua baada ya kuboresha bidhaa, huduma au uzalishaji na utendaji kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya CAPS LTD, Peter Marealle ameipongeza TBS kwa kuendelea kuwapa ushirikiano watoa huduma wa bidhaa nchini, wazalishaji na wauzaji wa bidhaa nchini kwani wao wamekuwa wakifanya vizuri na kuwafanya kutambulika ndani na nje ya nchi kupitia ubora wa bidhaa ambazo wanazizalisha na kuuza.
Social Plugin