Na Zena Mohamed,Dodoma
Meja Jenerali na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)Rajabu Mabele amesema
Uzalishaji wa mazao, ufugaji wa kisasa, na mbinu za uendelezaji wa ardhi ndizo zinazofanya JKT kupata tuzo mara kwa mara katika maonesho ya wakulima maarufu kama nanenane.
JKT limeshinda tuzo ya jumla kwenye maonesho ya wakulima nanenane 2024 yaliyofanyika kitaifa Dodoma kutokana na ufanisi wake katika kilimo na uthibitisho wa juhudi zake katika kuboresha uzalishaji wa mazao na kuleta maendeleo ya kilimo nchini.
Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo Jijini hapa Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Agosti 8,2024 na kueleza kuwa ushindi walioupata katika maonesho hayo yanatokana na juhudi, bidii na maarifa yaliyonayo jeshi hilo.
“Tunajivunia sana kwa sababu tumeweza kushinda tuzo kwenye maonesho haya muhimu,tuzo hii ni ushindi wa pamoja tunaosherehesha juhudi za pamoja zilizowekwa na askari wetu, wahandisi wetu, na wakulima wetu,katika kipindi chote cha maonesho, tumepata fursa ya kuonyesha namna JKT inavyoweza kuchangia katika kuboresha kilimo kupitia mbinu za kisasa na matumizi bora ya teknolojia.
“umeonyesha mifano ya mafanikio katika Uzalishaji wa mazao, ufugaji wa kisasa, na mbinu za uendelezaji wa ardhi ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya kilimo nchini,kwa ujumla tuzo hii inatupa motisha na nguvu zaidi ya kuendeleza kazi yetu ya kujenga taifa kupitia kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, “amesisitiza na kuongeza kuwa;
“Tunatambua kwamba mafanikio haya hayangewezekana bila ushirikiano wa karibu kati yetu na wakulima pamoja na wadau wote wa kilimo,tunawaahidi kuwa tutendelea kuweka mikakati ya kuimarisha kilimo, kutoa mafunzo, na kuendeleza teknolojia zinazosaidia kuongeza tija na ubora wa mazao na kuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya nchi yetu, “amesema.
Mbali na hayo Mkuu huyo wa JKT ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia kwa msaada na ushirikiano wake thabiti na kuahidi kuwa Jeshi hilo litaendelea kushikamana, kujitolea, na kuhakikisha kuwa linaleta mabadiliko chanya katika sekta hiyo kwa maslahi ya uchumi wa taifa .
“Hakuna ushindi unapotikana bila bidii,tulidhamiria kuifanya kazi hii, tulidhamiria kuhakikisha tunashinda, hakuna ushindi unakuja bila bidii, sisi tumeonesha bidii,tulionesha Nia Kwenye sekta zote za kilimo, mifugo na uvuvi ambapo Kwenye kilimo, tumekuwa tukifanya kilimo cha kisasa kupitia mazao ya chakula, biashara na Mazao ya kimkakati ambayo yanatumika kama shamba darasa kuwafundisha Vijana wanaopatiwa Mafunzo ya JKT katika Vikosi vyake vyote, “amesema.
Amezungumzia pia kwa upande wa mifugo kuwa JKT limekuwa likifuga n’gombe, Mbuzi, Kuku, Bata na mifugo mingine lakini pia limeanzisha teknolojia ya ufugaji wa samaki kwa njia mbalimbali ikiwemo Vizimba, Matanki ambapo mfugaji anatumia eneo dogo na kupata faida kubwa.
Social Plugin