Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAHITIMU NELSON MANDELA WAASWA KUTOA HUDUMA BORA KWA JAMII

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Balozi Maimuna Tarish akiongea na wahitimu na wageni waalikwa wakati wa Mahafali ya 10 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika Agosti 29, 2024 Kampasi ya Tengeru Arusha.

.......

WAHITIMU 92 wa Shahada za Uzamivu na Umahiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wameaswa kutatua changomoto katika jamii , sekta za uzalishaji pamoja na sekta ya huduma ili kuleta tija zaidi.

Hayo yalisemwa Agosti 29, 2024 Jijini Arusha na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Taasisi hiyo. Balozi Maimuna Tarish wakati wa Mahafali ya 10 ya kutunuku wahitimu hao shahada za Uzamivu (PhD) na Umahiri (Masters).

"Naamini mtachangia katika kuleta maendeleo endelevu kama kauli mbiu yetu isemayo taaluma kwa jamii na viwanda iendelee kuwa mwanga na mwongozo katika maeneo yenu ya kazi"

Alisisitiza kuwa, mafanikio si kipimo cha yale unayojua bali ni namna unavyotumia kile unachokijua hivyo nendeni mkatumie maarifa na ujuzi mlioupata katika kujenga Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.

Alisema, taasisi hiyo imejipambanua katika maeneo mbalimbali ikiwemo uhamilishaji wa teknolojia haswa katika ubunifu na utafiti unaozingatia maendeleo ya viwanda na changamoto za wananchi.

Alisema taasisi hiyo, imeendelea kutekelezeka mradi wa hosteli za kina mama wenye watoto wadogo na wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo sasa mradi huo umefikia asilimia 60 katika ujenzi wake.

Naye Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Maulilio Kipanyula alisema taasisi hiyo itaendelea kuwa kitovu cha maendeleo ya sayansi uhandisi, teknolojia na ubunifu katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alisema mahafali hayo yana jumla ya wahitimu 92 kati yao wanawake ni 29 na wanaume ni 63 ambapo wahitimu 17 kati yao sawa na asilimia 18 ni wanafunzi wa kigeni kutoka nchi za Kenya, Ghana, Uganda, Burundi,Malawi ,Rwanda, Sudani Kusini na Nigeria.

Aliongeza kuwa kati ya wahitimu 64 walitunukiwa shahada mbalimbali za Umahiri huku wahitimu 28 walitunukiwa shahada za Uzamivu ambazo ni matunda ya kazi nzuri zinazofanywa na Shule Kuu Sayansi Uhai na Uhandisi Biolojia (LiSBE), Shule Kuu Sayansi ya Malighafi Nishati, Maji na Mazingira (MEWES) na Shule Kuu ya Hisabati, Sayansi na Uhandisi wa Ukokotoaji na Mawasiliano (CoSCE).

"Nashukuru Bodi ya Mikopo ya Elimu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi na wadau kutoka mashirika ya Maendeleo ikiwemo Beni ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika , Serikali ya Ujerumani na wadau wengine kwa kuendelea kusaidia wanafunzi kwenye hatua mbalimbali za masomo yao " alisema Prof. Maulilio.


Prof. Gabriel Shirima Mlau wa Mahafali ya 10 ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela akiongoza maandamano wakati wa sherehe za mahafali Agosti 29, 2024 Kampasi ya Tengeru Arusha.


Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Bw. Omari Issa ( Katika mwenye Kofia nyekundu) akiwa na viongozi wa Taasisi wakati wa Sherehe za Mahafali ya 10 yaliyofanyika Agosti 29, 2024 katika Kampasi ya Tengeru Arusha.


Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Balozi Maimuna Tarish akiongea na wahitimu na wageni waalikwa wakati wa Mahafali ya 10 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika Agosti 29, 2024 Kampasi ya Tengeru Arusha.


Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Bw. Omari Issa akiwatunuku Wahitimu Shahada ya Uzamivu wakati wa Mahafali ya 10 ya Taasisi hiyo Agosti 29, 2024 katika Kampasi ya Tengeru Arusha.


Wahitimu 92 wa Shahada ya Umahiri na Uzamivu kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela katika Mahafali ya 10 ya Taasisi hiyo Agosti 29, 2024 katika kampasi ya Tengeru Arusha.


Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Balozi Maimuna Tarish (Kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza Prof. Lughano Kusiluka ( kushoto) wakati wa mahafali ya 10 ya taasisi hiyo Agosti 29, 2024 Kampasi ya Tengeru Arusha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com