NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo wamejengewa uelewa kuhusu kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na kuzichambua kwa mtazamo wa kijinsia hasa zile ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), Mwasilishaji Deogratius Temba amesema wananchi wanatakiwa kuelewa kanuni za uchaguzi ili waweze kushiriki vizuri kwenye mchakato wa uchaguzi kwa kuhakikisha wanafuata taratibu za uchaguzi.
Amesema sehemu ya kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 inaeleza kuhusu matangazo ya uchaguzi, usimamizi wa uchaguzi, na maelekezo muhimu kuhusu uchaguzi ambapo muhimu kuangalia jinsi kanuni hizi zinavyowezesha ushiriki wa wanawake na kuzingatia haki za kijinsia.
Amesema miongoni mwa kanuni hizo imeeleza kuhusu uandikishaji wa wapiga kura utaanza siku arobaini na saba kabla ya uchaguzi, na utachukua siku kumi.
"Uandikishaji ukifanyika kwa muda mrefu na sehemu inayofikikakirahisi, wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu, ikiwa hatuzingatii muda na mazingira kundi kubwa litakaloshindwa kujiandikisha ni wanawake". Amesema
Aidha amewataka vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ili waweze kuonesha uwezo wao wa kuongoza na kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Social Plugin