Na Christina Cosmas, Morogoro
WAZAZI nchini wamehimizwa kuzingatia maadili kwa Watoto kwa kutunza na kuhuisha tamaduni wao ili kuwafanya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha
Mwenyekiti wa Michezo ya Jadi kutoka Manispaa ya Morogoro Hilary Kunambi anasema hayo leo wakati akifungua siku ya utamaduni inayofanyika kwenye shule ya awali na msingi ya Uzima Academy iliyopo mkoani hapa ambapo alisema Watoto wengi huangalia televisheni na kutoelekezwa maadili na tamaduni zao.
Hivyo Kunambi anazishauri shule mbalimbali mkoani hapa na nchini kwa ujumla kuiga mwelekeo huo wa kuanzisha siku ya utamaduni kwenye shule zao ili kuwafanya vijana wadogo kujifunza utamaduni kulingana na mikoa wanayotoka ili kutopoteza asili zao.
Naye Mwenyekiti wa wazazi wa shule hiyo Emmanuel Mwakatobe amewataka wazazi kuwaweka wazi Watoto wao kulingana na tamaduni zilizopo nchini sababu Tanzania ni nchi yenye tamaduni nyingi na nzuri za kufuatwa ikiwemo mavazi, malazi, vyakula na hata nyimbo ambazo nyingi huimbwa wakati wa mavuno na sherehe zenye maadili mema kwa jamii.
Anasema ikiwa Watoto watapata uelewa wa kitamaduni mapema itawasaidia kutambua vyakula vya asili vinavyotakiwa ili waweze kula na pengine kupunguza magonjwa yanayoiandama jamii kwa sasa.
Naye Mkuu wa shule hiyo Leo Hyera anasema lengo kuu la kuanzisha siku hiyo ya utamaduni ambayo itafanyika kila mwaka shuleni hapo yenye kauli mbiu isemayo “asili yetu maisha yetu” ni kuhuisha utamaduni na kukuza lugha ya Kiswahili nchini.
Hyera anasema wameamua kufanya siku hiyo baada ya kuona Watoto wanapoteza Kiswahili ambacho ndio utamaduni wa kwanza wa mtanzania ambapo tamaduni za nje zimeonekana kujaribu kuua utamaduni wa mtanzania.
Anasema kupitia siku hiyo ya utamaduni watahakikisha Watoto wanajifunza tamaduni nzuri na kuwaelimisha namna ya kutoathirika na tamaduni zenye maadili potofu ikiwemo ukeketaji.
Naye mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao Esther Lwendo amefurahishwa na kuanzishwa kwa siku ya utamaduni shuleni hapo ambayo itawasaidia Watoto kujifunza zaidi kupitia nyumba za makabila zilizojengwa.
“kupitia nyumba za makabila zilizojengwa zimenifurahisha kwani huwafanya Watoto wafunguke na kujua utamaduni wa asili zetu, wasikae tu kujua mambo ya nje na kusahau mambo yetu na asili zetu, sababu kuna siku nilimwambia mwanangu kuhusu kibatari akanihoji ni kitu gani, lakini leo nilipokiona nikaenda nikamwambia njoo uone kibatari, nikamuonesha, na pia nilimwambia kuhusu birika nae akashangaa na pia leo nilipoliona nikampeleka kuliona pia akanielewa, hili ni somo zuri” anasema .
Naye mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo Janeth Mwaisumo anasema amefurahishwa na mambo ya utamaduni waliyofundishwa ambapo amejifunza kucheza ngoma za asili na kupika mboga za asili hata kama hajafika kijijini kwao.
Sherehe hizo zimeenda sambamba na maonesho ya mavazi ya makabila, ngoma, historia ya makabila sambamba na uwepo wa nyumba za misonge za asili ya wasukuma, wahaya na wachaga kwenye eneo la shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi kuendelea kujifunza.
Social Plugin