Na Christina Cosmas, Morogoro
KITENDO cha wazazi kushindwa kuwa jirani na watoto zao katika malezi kimetajwa kuwa ndio njia ya ongezeko la mmonyoko wa maadili, vitendo vya ukatili pamoja na unyanyasaji kwa watoto vinavyotokana na watoto kutosikilizwa na kukosa malezi bora.
Akizungumza katika kuhitimisha mashindano ya Mtoto Bomba Diwani wa Kata ya mji mpya Manispaa ya Morogoro Emmy Kiula amesema ipo haja ya kuandaa makongamano mbalimbali yatakayoweza kuwakutanisha watoto na kuwapa elimu juu ya ukatili unaofanywa na kusababisha kuharibika kwa kizazi Bora.
Aidha amesema kuwa hali kwa sasa siyo salama kwani watoto wengi wanafanyanyiwa vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kukosa sehemu ya kwenda kutoa taarifa kwani wazazi wengi hawana muda wa kuwasikiliza watoto wao.
Kwa Upande wake mkurugenzi wa mashindano ya mtoto bomba Paschal Elias amesema kwa kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Dkt Samia Suluhu Hasani wameunga Mkono na kuanzisha mashindano haya yenye lengo la kuinua vipaji pamoja na kutoa elimu kwa watoto dhidi ya ukatili
Hata hivyo ameiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali kushirikiana katika mashindano haya ikiwa lengo kuu ni kupunguza na kumaliza ukatili kwa watoto pamoja na kuandaa na kutengeneza kizazi kilicho Bora
Naye Koplo wa polisi (CPL) Suleiman Ibrahim Kova wa Dawati la Jinsia amewataka wazazi kukaa na watoto wao na kuacha kuwategemea walimu wao kwa asilimia kubwa kwani mtoto ana nafasi kubwa ya kumweleza mzazi wake juu ya mambo mabaya anayofanyiwa
Mashindano ya mtoto bomba yalianza tangu julai 1 na kutamatika Agosti 24 huku shule mbalimbali kutoka Mkoani Morogoro zikishiriki na yanatarajia kufanyika tena Disemba 2024 yakiambatana na matukio mbalimbali kama kwenda kutoa msaada katika vituo vya watoto yatima mkoani Morogoro
Mwisho...
Social Plugin