Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na wananchi kwenye banda la kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kwenye maonesho ya nanenane viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, DODOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana ametaja mikakati mbalimbali ya kufikisha huduma za kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria (Mama Samia Legal Aid Campaign) na kutangaza namba ya simu ya kupiga ili wananchi wapate huduma na kuondokana na Mawakili vishoka.
Aidha, wizara hiyo inatarajia kuanisha wasaidizi wa kisheria wanaopatikana kwenye wilaya na Mikoa ili kurahisisha wananchi kusaidiwa kupata haki zao.
Pamoja na hayo, amesema kampeni hiyo inajipanga kuanza kuambatana na kliniki ya ardhi iliyopo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi.
Akizungumza leo kwenye maonesho ya nanenane alipotembelea banda la kampeni hiyo kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Waziri huyo amesema kutokana malalamiko ya migogoro ya ardhi kuwasilishwa kwa wengi kwenye kampeni hiyo atakutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili wataalamu wa sheria kuambatana na kliniki ya ardhi.
Kadhalika, ameelekeza watendaji wa wizara kuainisha kila wilaya wasaidizi wa kisheria wanapatikana wapi kwenye maeneo yao ili wananchi warahisishiwe kupata huduma za kisheria kupitia kampeni hiyo.
“Tunakuja na Directory itakayoonesha kila wilaya na mkoa nani anatoa huduma ipi na itasaidia mtanzania popote alipo kuona pale ni nani anatoa huduma kwenye eneo husika, kwenye Kijiji au kata tunataka kutambuana nani anatoa huduma ya msaada wa kisheria bure,”amesema.
Ameongeza kuwa “Kama mnavyofahamu Rais ametupa maelekezo na bajeti tuwafikie watanzania milioni 61 wanahitaji msaada wa kisheria maeneo mbalimbali na Wizara ya Katiba na Sheria ina jukumu la msingi kuwafikia watanzania na kwasasa tumekuja na kituo cha huduma kwa mteja ambacho mwananchi anaweza kupiga simu na hii ndo kutekeleza falsafa ya 4R za Rais na hapa tunafanya mageuzi ya mifumo ya kisheria.”
Ameeleza kuwa Wizara hiyo inawakaribisha wananchi na milango ipo wazi ili wapate msaada wa kisheria bure kwa kupiga simu 0262160360 ili kupata ushauri wa kisheria na kuwasaidia kuwaepusha wananchi na vishoka.
“Kuna maeneo kuna wanasheria vishoka na tumebadili sheria wale vishoka wanaotoa ushauri wa kudanganya sheria inakataza na watachukuliwa hatua kali kwa wale ambao ni vishoka,”amesema.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, amesema kwa siku saba katika maonesho hayo malalamiko ya watu 767 yamesajiliwa huku migogoro ya ardhi ikiongoza.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Wizara hiyo, Ester Msambazi, amesema wananchi wengi kupitia maonesho hayo wamefika kupata ushauri na elimu ikiwamo makundi ya wanafunzi wamepatiwa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na haki zao.
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na wananchi kwenye banda la kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kwenye maonesho ya nanenane viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Social Plugin