Na WMJJWM-Dodoma
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu zimeweka Mipango na mikakati ya kuhakikisha watoto wanapata Malezi Bora ili kuwa na Taifa lenye maadili katika hatua ya kuelekea kwenye umri wa ujana.
Hayo yamebainika wakati wa makabidhiano ya vifaa vya mafunzo ya vitendo ikiwemo vyerehani thelathini (30) kwaajili ya Watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Agosti 16, 2024 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Ridhwani Kikwete amesema Wizara itashirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii katika kuhakikisha watoto wanapofikia hatua ya ujana wanakuwa katika malezi ambayo yatawasaidia kuwa na Vijana bora katika Taifa.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali wanaotoa malezi kwa watoto katika Makao ya Watoto kuwapa fursa watoto kupata kujifunza stadi mbalimbali za kazi ili ziwasaidie kuendeleza maisha yao ya baadae mara watakapofikia umri wa kuondoka katika Makao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema Wizara ina mipango mbalimbali inayolenga kuwajenga watoto katika hatua za Malezi na Makuzi, kuelekea hatua za kufikia ujana.
Ameongeza kuwa jambo la kuwasaidia watoto hao ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha watoto wanakuwa na mazingira mazuri katika ukuaji wao kwa kupata fursa mbalimbali ikiwemo elimu na ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao.
"Sisi Wizara tunaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau wengine ili kuhakikisha watoto wetu wanaolelewa katika Makao haya na Makao mengine wanapata fursa za kujifunza stadii mbalimbali za kazi zitakazowasaidia kujitegemea wakati wa ujana" amesema Naibu Waziri Mwanaidi