OFISA Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati, Juma Singano,akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la EWURA katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna_DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa rai kwa wananchi ambao hawaridhishwi na huduma wanazozipata za nishati na maji kuwasilisha malalamiko yao ili kupata haki zao.
Ofisa Huduma kwa Wateja wa EWURA Kanda ya Kati, Juma Singano, amesema Mamlaka hiyo hupokea na kushughulikia malalamiko mbalimbali baina ya mtoa huduma na mtumia huduma zote zinazodhibitiwa na EWURA.
“EWURA ina utaratibu maalum wa kupokea na kushughulikia migogoro na malalamiko yanayotokana na huduma zinazodhibitiwa katika sekta za nishati na maji ambapo mteja hujaza fomu kubainisha masuala yanayomtatiza kama ankra za maji au kucheleweshewa kuunganishiwa huduma, ambapo utaratibu unamtaka mteja kabla ya kupeleka malalamiko EWURA kwanza ayawasilishe kwa mtoa huduma, kwa mfano kwa Dodoma masuala ya maji mteja atawasiliha DUWASA kabla ya kufikisha suala lake EWURA.” alisema.
Singano amesema; kwa mteja aliyeomba huduma ya kuunganishiwa maji mathalani, akishalipia gharama za maunganisho, mamlaka ya maji inapaswa kumpatia huduma ndani ya siku saba na endapo siku hizo zikipita bila maunganisho ya maji kwa mteja, mkataba wa huduma kwa mteja kati ya mamlaka ya maji na mteja unamtaka kulipwa Sh.15,000 kwa siku ya nane na kuanzia siku ya tisa na kuendelea, endapo hilo halikufanyika, mteja anatakiwa kulipwa sh.5.000.
Hivyo, ni muhimu kwa mtumiaji huduma majisafi na usafi wa mazingira kuhakikisha anapata mkataba wa huduma kwa mteja kutoka mamlaka ya maji inayomhudumia ili kujua haki na wajibu wake pamoja na viwango vya ubora wa huduma za maji na usafi wa mazingira ili anapopata changamoto achukue hatua stahiki ikiwemo kuwasiliana na mamlaka ya maji endapo hataridhika na hatua zilizochukuliwa na mtoa huduma ana haki ya kuwasilisha malalamiko yake EWURA ili yashughulikiwe.
Aidha, Singano ameeleza kuwa katika maonesho ya Nane Nane mwaka huu, wananchi zaidi ya 300 waliotembelea banda la EWURA wamepata elimu ya namna ya kuwasilisha malalamiko yanayotokana na shughuli zote zinazodhibitiwa na EWURA.
“Tukipokea lalamiko la mteja, tunamtumia mtoa huduma wito wa kutoa utetezi na ndani ya siku ya 21 mtuhumiwa anatakiwa awe ametoa utetezi wake na mlalamikaji atataarifiwa endapo ataridhishwa na utetezi uliowasilishwa na mtoa huduma, mteja anaruhusiwa kuondoa shauri na kama hataridhika EWURA huitisha shauri ndani ya siku 30 za kazi kusikiliza na kutoa suluhu”.alisema
OFISA Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati, Juma Singano,akizungumza kwenye banda la EWURA wakati wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
OFISA Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati, Juma Singano,akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la EWURA katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Social Plugin