Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imehitimisha kambi maalum ya uchunguzi na upandikizaji wa meno bandia ambapo wagonjwa takribani 30 wamefanyiwa matibabu ya kupandikiza meno bandia kwa njia ya kisasa, huduma ambayo imefanyika kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Umma nchini.
Kwa mujibu wa Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno Dkt. Peter Shempemba zaidi ya wagonjwa 201 walifanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo na kubainika kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoboka au kuoza kwa meno, magonjwa ya fizi, vibogoyo na mpangilio mbaya wa meno yao.
Dkt. Shempemba ameanisha kuwa baada ya uchunguzi huo kila mmoja alipatiwa matibabu stahiki kulingana na changamoto walizonazo na kwa sasa wanaendelea vizuri.
Dkt. Shempemba ameongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 66 wanapoteza meno kwa sababu mbalimbali hivyo mahitaji ya kurudisha meno yaliyopotea ni makubwa ndio maana hospitali hiyo imekuja na huduma hiyo inayotumia teknolojia ya kisasa kabisa ili kuwasaidia Watanzania wengi kwa gharama nafuu hapa hapa nchini.
Hospitali ya Taifa Muhimbili imeendela kuanzisha huduma za ubingwa bobezi ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani hapa nchini hivyo kuwapunguzia wananchi usumbufu na gharama za kwenda kutafuta matibabu hayo nje ya nchi.
Social Plugin