CCM TANGA YAFANYA DUA MAALUMU KUMUOMBEA MAREHEMU ALI KIBAO ALIYEKUWA KADA WA CHADEMA


 Na Hadija Bagasha Tanga, 

Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Tanga kimefanya dua maalumu ya kumuombea marehemu Ali Kibao aliyekuwa kada wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema aliyefariki hivi karibuni baada ya kutekwa na watu wasiojulikana na kisha kuuwawa kikatili na kutupwa kwenye eneo la Ununio jijini Dar e salaam

Mwenyekiti wa CCM  Mkoa Tanga Rajab Abrahaman Abdallah ameungana na watanzania wengine kulaani vitendo vya baadhi ya watu kutekwa na kuuwawa kikatili. 

Mwenyekiti Rajab ametoa kauli wakati wa dua maalumu iliyoandaliwa na chama cha mapinduzi ccm Mkoa Tanga iliyofanyika katika msikiti wa Ijumaa jijini Tanga ya kumuombea marehemu Ali Kibao aliyekuwa kada wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema aliyefariki hivi karibuni baada ya kutekwa na watu wasiojulikana na kisha kuuwawa kikatili na kutupwa kwenye eneo la Ununio jijini Daresalaam. 

Katika dua hiyo maalumu Mwenyekiti Rajab amesema kwamba wameguswa na msiba huo hivyo wanaungana na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na watanzania wengine kwamba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini wale wote waliohusika na mauaji hayo. 

Mwenyekiti Rajab amewataka watanzania kukemea na kufichua matendo maovu na ya kuhalifu yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini ambapo matukio hayo yamekuwa yakileta madhara makubwa kwa jamii. 

"Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maamuzi makubwa aliyoyafanya juu ya jambo hili niwaombe sana watanzania wote kwa ujumla ikiwemo sisi watu wa Tanga hususani wa dini mbalimbali tuendelee kumuombea Rais wetu na kukemea mambo machafu ambayo yamekuwa yakifanyika kwenye nchi yetu, "alisisitiza Rajab. 

"Mara nyingi nchi yetu huwa kuna vipindi inapitia katika mambo magumu sana mtakumbuka miaka ya nyuma kidogo kulikuwa kuna wimbi kubwa la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)  watu wanadanganywa na waganga ukiwa na kiungo cha Albino wewe ni tajiri kumbe sio kweli ni ukatili tu ulikuwa ukifanyika, "alisema

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Tanga,  Mkuu wa Wilaya ya Tanga Japhari Kubecha ameishukuru Familia ya marehemu kwa kuridhia kufanyika kwa dua hiyo huku akisema serikali ya Mkoa huo itaendelea kupambana na uhalifu wa aina yeyote ili kuhakikisha wananchi wanaishi mahala salama pamoja na mali zao. 

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Mkoa Tanga Juma Luwuchu amewaasa wanafamilia kuendelea kuwa subira katika kipindi chote ambacho uchunguzi unaendelea kufanyika ili kubaini waliohusika na uhalifu huo. 

Akuzungumza kwa niaba ya familia ya marehemu Ali Kibao mmoja wa familia hiyo Mukhusin Hemed ameishukuru serikali kwa kuungana nao katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.    



















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post