GRUMETI FUND YATOA ELIMU KWA ZAIDI YA WANAFUNZI 1000 WILAYANI BUNDA - MARA

SHIRIKA la Grumeti Fund  kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imewaleta pamoja Wanafunzi wa kike 688 na wakiume 610 kutoka katika shule za Kunzugu, Sizaki na Paul Jones sekondari zilizopo Wilayani Bunda, kwa lengo la kutoa Elimu sambamba na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike na kiume pamoja na utatuzi wake ili kujenga jamii yenye usawa miongoni mwa vijana wa jinsia zote.

Katika kongamano lililofanyika kwa siku mbili katika shule ya Sekondari Kunzugu yakihusisha wanafunzi wa kike na kiume, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumeti Fund Bi. Frida Mollel amesema  lengo la Grumeti Fund kufanya kongamano hilo ni kuwaelimisha  vijana wa kike na kiume kutambua thamani yao sambamba na kuwajengea uwezo wa kujiamini na kufikia ndoto zao huku akiwataka kumtanguliza Mungu katika kila jambo kwani ndio msingi wa mafanikio.

"Vijana wengi sasa wametumbukia katika tabia hatarishi ambazo kupitia tabia hizo ni ngumu kufikia ndoto zenu, ili muweze kufikia ndoto zenu na kuwa vijana wakutegemewa katika familia na taifa Kwa ujumla, mambo matatu muhimu ambayo ninyi kama vijana mnatakiwa kuyaweka mbele kwanza ni kumcha Mungu kwasababu ndio chanzo cha maarifa , pili, kujitambua na kujiamini, na kufanya bidii katika masomo.  Grumeti Fund, tumekuja kuwatia moyo kuwa unaweza kuwa mtu yeyote endapo utamtanguliza Mungu, ukitambua thamani yako na ukijiamini na kufanya bidii asitokee mtu atakayekwambia kuwa huwezi, nawataka mfahamu kwamba mnaweza",amesema.

Aidha, Bi. Frida amewataka vijana hao kutotumbukia katika matumizi mabaya ya utandawazi na kuwataka vijana hao kuitumia mitandao ya kijamii katika namna itakayowaongezea ujuzi katika kuzitimiza ndoto zao.

Katika kongamano hilo shirika la Grumeti Fund imetoa Mipira na jezi za mpira Kwa shule zote tatu zilizoshiriki kwa wanafunzi wa kiume na  msaada wa taulo za kike  zinazoweza kutumika  kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu (reusable pads) kwa wanafunzi wa kike 688 zenye thamani ya Shilingi 9,632,000/- katika shule za sekondari Kunzugu, Paul Jones na Sizaki.

Naye mgeni rasmi  katika kongamano la wasichana Bi. Pelesia Manyama ambaye ni Katibu wa chama cha Walimu, amewataka wasichana kuwekeza katika kumcha Mungu kwani Kwa Mungu ndipo msaada wa matatizo yote unapatikana.

"Niwaambie kuwa ukimcha Mungu utaepuka mambo mengi mabaya, hata sisi tulivyo hivi ni kwasababu tuliwekeza katika kumcha Mungu na bado tunamtegemea yeye hadi sasa, kwani mwanafunzi bila kumtegemea Mungu hautafika popote, dunia na tamaa zake zitakumeza. Ili kufanikiwa katika masomo yako jitahidi sana kuwa na hofu ya Mungu pamoja na kuwekeza katika kumcha Mungu" Jiepusheni na marafiki wabaya na mambo yasiyo na tija",amesema Bi. Pelesia Manyama.

Kwa upande wake  mkufunzi kutoka  chuo cha Afya Kisare Mwl. Restuda Murutta akitoa Elimu ya uzazi kwa wanafunzi wa kike amewaasa kuzingatia usafi wawapo katika siku za hedhi na  kuwataka kuzitumia taulo za kike zilizotolewa na Grumeti Fund kwa usahihi sambamba na kuepuka vishawishi vitakavyo waingiza katika kufanya mapenzi katika umri mdogo na mwisho kupelekea ndoa za utotoni.

“Usafi wakati wa hedhi ni muhimu sana kwani utaepuka magonjwa mbalimbali, lakini pia inasikitisha binti anaumri chini ya miaka 18 ameshaanza kujiingiza kwenye mahusiano ya ngono kitu ambacho sio salama, kabla ya kuingia kwenye mambo hayo kwanza jiulize je ni umri sahihi wa kuingia kwenye mambo hayo ukishapata jibu acha", amesema Bi. Restuda

Naye aliyekuwa Mgeni rasmi katika kongamano la wanafunzi wa kiume  anayehudumia idara ya vijana katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Emmanuel Samuel Sitta amewaasa vijana wa kiume kujitambua kuwa wao ni wanaume na wameumbwa na Mwenyezi Mungu kama wanaume Kwa makusudi.

"Siku hizi imezuka tabia ya wanaume kutamani kufanya mambo ya jinsia ya kike, niwaambie kuwa wewe umeumbwa na Mungu kama mwanaume hivyo unatakiwa kufanya yale yaliyowekwa na Mungu ili yafanywe na wanaume na si vinginevyo ", amesema Mchungaji Sitta.

Nao miongoni mwa wanafunzi wa kike na kiume waliopata mafunzo wameishukuru kampuni ya Grumeti Fund kwa namna wanavyowajali na kuwathamini vijana wa kike na kiume katika kujenga jamii bora yenye usawa na kuahidi kuyaweka katika vitendo mafunzo hayo na kusambaza elimu kwa wengine.

Kwa takribani miaka saba kampuni ya Grumeti Fund imekuwa ikitoa elimu ya kijinsia kwa wanafunzi wa kike na kiume katika shule za sekondari mbalimbali Wilayani Serengeti na Bunda ambapo tangu mwaka 2017 hadi awamu hii ya tatu  ya kongamano hili kwa Mwaka 2024  imefanikiwa kutoa elimu ya kijinsia kwa wasichana 12,397 na kutoa taulo 12,397  kwa kila binti anayeshiriki mafunzo hayo, huku ikifanikiwa kutoa mafunzo kwa wavulana zaidi ya 6,274 tangu mwaka 2021 hadi awamu hii  ya tatu ya kongamano la Mwaka 2024 na kutoa zawadi za jezi na mipira  kwa kila shule iliyoshiriki kwenye kongamano.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post