Na Christina Cosmas, Morogoro
Mizinga ya nyuki 135 inatarajia kugawiwa kwa wananchi wa eneo la Kibaha na Kisarawe ili kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kwenye mto Ruvu na mto Kizinga.
Mkurugenzi waTaasisi ya uhifadhi wa mazingira na kilimo (Agriwezesha) Deogracia Ignas amesema hayo wakati wa kumbukizi ya miaka 5 ya taasisi hiyo ambapo alisema mizinga hiyo itagawiwa kwenye vikundi 9 vyenye wastani wa watu 10 hadi 15 na kuwa sehemu ya shamba darasa la watu kujifunza.
Ignas anasema tayari wameshawapa mafunzo wanufaika ambapo wanalenga kufanya mambo ya uhifadhi katika mto Ruvu na Kizinga ili kukomesha watu kufanya shughuli zisizo rafiki kwenye mito na kuwapa shughuli rafiki ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
Amezitaja kazi zinazofanywa na kuharibu mazingira kuwa ni pamoja na ukataji wa mkaa kwa ajili ya kuni za biashara na uchomaji wa mkaa ambapo mizinga hiyo itawasaidia kuwaingizia kipato.
Naye Balozi wa mazingira kutoka ofisi ya makamu wa Rais Muungano na mazingira Chage Alex Chage anasema jamii inapaswa kuona haja ya kuendeleza utunzaji wa mazingira utakaosaidia dunia kuepuka kufikia kwenye ongezeko la juu ya joto la kiasi cha nyuzi joto 1.5 mwaka 2050.
Chage anasema kwa mujibu wa takwimu za kimataifa kwa sasa kiwango cha juu cha joto kimefikia nyuzi joto 1.2 ambayo pia haitakiwi kuzidi jamii inapaswa kuwa macho katika kusimamia shughuli za utunzaji wa mazingira na kujiepusha na kufika kwenye matokeo ya mabadiliko ya tabianchi.