Akizungumza leo Jumanne Septemba 17,2024 kwenye hafla ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi, hafla ambayo pia imeadhimisha miaka 60 ya Jeshi hilo, Rais Samia aliwapongeza askari wa polisi kwa kazi yao kubwa ya kulinda amani na utulivu wa taifa letu.
Rais amethibitisha kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Katika hotuba hiyo ya kihistoria, Rais Samia aliweka wazi kuwa Tanzania ni nchi inayojitegemea na yenye hadhi, na hivyo haiwezi kuamriwa na watu wa nje kuhusu jinsi ya kuendesha masuala yake ya ndani.
Alikemea vikali kauli za kibaguzi zilizotolewa na baadhi ya balozi za kigeni baada ya kifo cha mwanachama wa Chadema, Ali Kibao. Alifafanua kuwa kauli hizo hazikutolewa kwa ridhaa ya serikali za balozi hizo, na akasisitiza kuwa balozi hizo zinapaswa kuheshimu mamlaka ya Tanzania kama vile balozi zetu zinavyoheshimu mamlaka za nchi nyingine.