Baadhi ya waombolezaji baada ya ajali ya moto
Nchi ya kenya imetangaza siku tatu za maombolezo ya Kitaifa kutokana na vifo vya wanafunzi 17 wa shule ya msingi ya Hillside Endarasha kufariki katika ajali ya moto iliyotokea katika shule hiyo.
Rais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombolezo ya kitaifa yatakayoambatana na bendera ya nchi hiyo pamoja na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitapepea nusu mlingoti katika Ikulu, vituo vyote vya kidiplomasia vya Kenya pamoja na ofisi zote za umma kuanzia Jumatatu, Septemba 9, 2024, hadi Jumatano, Septemba 11 .
Awali baada ya kuripotiwa kutokea kwa tukio hilo Rais Ruto alitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto wao, huku akiwaombea majeruhi kupona kwa haraka.
Aidha Rais Ruto ameagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na watakaobainika kuhusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, tayari timu ya uchunguzi imeshafika katika eneo hilo na inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo ili hatua zingine ziweze kufuatwa.
Wakati akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo, Dk Resila Onyango alisema tukio hilo pia limesababisha majeraha kwa watoto 14 ambao wamepelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijajulikana.
Social Plugin