Ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar hivi karibuni inaonesha jumla ya matukio 165 ya ukatili wa kijinsia yaliripotiwa kwa mwezi Julai 2024, ambapo waathirika wengi walikuwa ni watoto. Ripoti inaonesha idadi ya watoto ni 142 sawa na asilimia 86.1 ya waathirika wote, ambapo wasichana walikuwa 115 sawa na asilimia 81.0 na wavulana 27 sawa na asilimia 19.0.
Hali hii inasikitisha na inahitaji kudhibitiwa na wadau wote wakiwemo Serikali, taasisi za jamiidini, wazee, walimu na watoto wenyewe kupewa elimu ya kujilinda na kujikinga dhidi ya watu waovu.
Wadau pia wanapaswa kuangalia upya ni kwa jinsi gani wanaweza kutatua changamoto zinazopelekea ongezeko la ukatili kwa watoto ambao ki msingi wanahitaji kulindwa kwa nguvu zote. Sheria ya Mtoto ya Zanzibar Na 6 ya mwaka 2011 inapinga udhalilishaji wa watoto wa aina yoyote ile ili kukuza ustawi wa watoto.
Aidha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (UNCRC) ya mwaka 1989 ambao umeridhiwa na nchi ya Tanzania ikiwemo Zanzibar unasisitiza kudumisha haki za mtoto ikiwemo ulinzi jambo linalopelekea kujenga jamii na Taifa lenye raia wenye kuheshimiana.
Hivi karibuni, tulishuhudia udhalilishaji wa watoto wasio na hatia uliofanywa na watendaji wa Manispaa ya Magharibi ‘A’, kwa kumkamata mtoto wa miaka miwili (2) na kumchukua pamoja na mlezi wake kwa kisingizio cha wazazi wa mtoto huyo kutolipa ada ya usafi, wakati wazazi wakiwa katika majukumu yao ya kikazi.
Jambo hili lilizua taharuki kwa familia ya mtoto huyo na jamii kwa ujumla, kwa vile ni kitendo kinachokwenda kinyume na haki za mtoto pamoja na haki za binaadamu. Kwa muktadha huo, TAMWA ZNZ inakemea vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto na inataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wale wote wanaokwenda kinyume na sheria.
Tunatoa wito kwa jamii kuwalinda watoto wetu na kuhakikisha hawakumbwi na vitendo vya udhalilishaji.
Imetolewa na kitengo cha Habari na Mawasiliano,
TAMWA ZNZ.
Social Plugin