TAMKO LA KUKEMEA VITENDO VYA KIKATILI VINAVYOENDELEA KUFANYWA KWA WATOTO KUFUATIA KIFO CHA MTOTO WA MIEZI SITA AMBAYE ALIFARIKI BAADA YA KUFANYIWA KITENDO CHA UBAKAJI NA ULAWITI MPAKA MAUTI SIKU YA JUMAPILI SEPTEMBA 1,2024.
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Vituo vya Taarifa na Maarifa na washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo tunaungana na wanaharakati wote kutoa tamko la kukemea vikali vitendo vilivyokithiri kwa watoto kufuatia kifo cha mtoto mwenye umri wa miezi sita kilichofanyika huko mkoani Dodoma Septemba 1.
Tukio hili la kikatili lililotokea na kumtambua baba mzazi wa mtoto huyo, Stephen Damas(38) kama mtuhumiwa wa kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kike mwenye umri wa miezi sita hadi kupelekea kifo.
Matukio haya yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka. Gazeti la Mwananchi la Ijumaa Julai 26 2024 ilitoa taarifa ya ripoti ya takwimu za uhalifu na usalama barabarani kama ilivyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania na kuchapishwa na ofisi ya taifa ya takwimu (NBS) kuwa; mwaka 2022 kulikuwa na matukio ya ukatili wa Watoto 12,163 na kuongezeka mwaka 2023 kufikia 15,301 ambalo ni nongezeko la asilimia 25.8.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 12(2) inasema: "Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.” Aidha, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka 1981, kifungu cha 130(2)(e) kinasema: "Mtu yeyote anayefanya kitendo cha kubaka, atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa adhabu kali kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 131." Kifungu cha 131(1) kinasema:"Mtu anayepatikana na hatia ya kosa la ubakaji atahukumiwa kifungo
cha maisha jela au kifungo cha muda usiopungua miaka thelathini."
TGNP inatoa wito kwa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka husika kuhakikisha kwamba vitendo hivi vinakomeshwa na adhabu kali za kisheria za mfano zinatolewa kwa watuhumiwa kwa wakati na haraka ili iwe fundisho kwa wengine.
TGNP inatoa wito kwa serikali, wadau mbali mbali na jamii kwa ujumla kushirikiana kutoa msaada wa kisaikolojia kwa familia hususani Mama mzazi Stella Gideon kufuatiwa mkasa huu wa kusikitisha ambapo kwa kiasi kikubwa atakuwa ameathiriwa na tukio hili.
Vilevile, TGNP inatoa wito kwa jamii nzima kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama, mashirika ya kiraia na wadau wote kuendelea kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na kudai mazingira salama na rafiki kwa watoto wetu kwani ndio msingi wa taifa la kesho.
Kwa pamoja tuijenge jamii inayozingatia haki, utu na usalama kwa wote.
Imetolewa na,
Lilian Liundi
Mkurugenzi Mtendaji
Mtandao wa Jinsia Tanzania-TGNP.
Social Plugin