Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFISA MTENDAJI MKUU WAZOHURU ATOA RAI KWA WATANZANIA KUACHA KUMKEJELI RAIS SAMIA



Na Dotto Kwilasa, Singida

Afisa Mtendaji Mkuu wa WazoHuru Media Group Ltd Ndg Mathias Canal,ametoa rai kwa watanzania kumtia moyo na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo makubwa anayoyafanya kwa ajili ya watanzania na kuacha kumbeza au kumkejeli.

Afisa Mtendaji huyo ameeleza hayo 19 Septemba 2024 kwenye mahafali ya 61 ya Shule ya Msingi Kiomboi-Bomani iliyopo Wilayani Iramba Mkoani Singida ambapo amesema maendeleo huja kwa kupeana moyo na kushirikiana.

Amesema kuwa Rais Samia ni mwanasiasa mstahimilivu na mwenye utulivu wa hali ya juu katika uongozi wake jambo linalozidi kuchochea na kusukuma maendeleo kila sehemu.
Akitolea mfano Kwenye Wilaya ya Iramba, Canal amesema kulikuwa na shule 4 za msingi na sasa zipo za msingi 111 ambapo za serikali ni 108 na shule binafsi ni tatu.

Kwa upande wa shule ya sekondari Wilaya ya Iramba kulikuwa na shule 1 na sasa zipo 29 ambapo za serikali ni 26 na za binafsi zipo 3.

"Wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961 kulikuwa na Chuo Kikuu kimoja pekee ambapo kwa sasa mambo yamebadilika kwani Serikali sasa imeimarisha sekta ya elimu na kuwa na vyuo vikuu 30 na vyuo vishiriki 12 mpaka sasa, " Ameeleza.

Canal ameeleza kuwa mwaka 2022 serikali ilifanya mapitio na Mabadiliko ya mitaala na Sera ya elimu ya mwaka 2014 hatimaye kuwa na toleo jipya la sera ya elimu ya mwaka 2023.
"Kwa ujumla katika sera hiyo ya elimu kutakuwa na mambo muhimu ikiwemo Kutoa elimu ujuzi badala ya taaluma pekee, na Elimu ya lazima itakuwa miaka 10 badala ya 7," Anasisitiza mkurugenzi huyo na mdau wa maendeleo hapa nchini.

Sambamba na hayo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda kwa kuja na wazo la ujenzi wa vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) ambapo Wilaya ya Iramba imepokea Bilioni 1.4 na ujenzi wa VETA unaendelea katika Kijiji cha Salala kata ya Old Kiomboi.

Hali kadhalika amempongeza Mbunge wa Jimbo la Iramba ambaye ni Waziri wa Fedha Mhe Dkt Mwigulu Mchemba kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo katika jimbo lake ambapo katika kipindi cha miaka minne 2020-2024 Wilaya ya Iramba imepokea Bilioni 6.682 kwa ajili ya sekta ya elimu.

Katika mahafali hayo Ndg Mathias Canal amechangia kiasi cha Shilingi 400,000 kwa ajili ya motisha kwa walimu, Mipira 6 na jezi jozi mbili. Mipira mitatu na jezi jozi moja kwa ajili ya mchezo wa mpira wa miguu (Football) na mipira mitatu na jezi jozi moja kwa ajili ya mchezo wa mpira wa pete (Netball).










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com