BALOZI wa Tanzania nchini Uganda Meja Generali Paulo Kisesa Simuli amesema kuwa asilimia 50 ya mabomba yatakayotumika kwenye mradi wa bomba la mafuta linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga Tanzania imeshakamilika hii ikiwa inazidi kuchochea kasi ya ujenzi kwa wakandarasi wa pande zote mbili ambao mpaka sasa wamefikia hatua nzuri.
Meja Simuli amebainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua na kutembelea kituo kikubwa cha Chongoleani Mkoani Tanga ambapo ameridhidhwa na kasi ya ujenzi inavyoendelea akiwapongeza wakandarasi wa vituo vyote vinavyopitiwa na mradi huo hapa nchini.
"Mabomba ambayo yameshaletwa yameshafikia nusu ya mabomba ambayo yatatandazwa kutoka Chongoleani mpaka Hoima tayari wameshafikia asilimia 50 mkandarsi amesema kuwa yakitandazwa yanaweza kufikia urefu wa zaidi ya Kilomita 700 na urefu wa kutoka hapa (Chongoleani) mpaka Hoima ni Kilomita 1443, kwahiyo ni matumaini yetu kwamba huu mradi utakamilika na hautalala", alisema Meja Simuli na kuongeza .
"Kwa hatua tuliyofikia nawashukuru na kuwapongeza sana wakandarasi wote, TPDC pamoja na wizara ya nishati ambao jambo hili wamelishikia bango bila kuwasahau wizara yetu ya mambo ya nje kwa kuendelea kudumisha mahusiano kwa nchi zote mbili ambayo yanatunufaisha katika nyanja ya kiuchumi"
"Mradi ni nzuri , wa kimakakati na wa kimaendeleo nimefika pale Kahama ambapo wanayafunika mabomba ili yaweze kutunza joto lakini pia kuna pampu zimewekwa kwaajili ya kusukuma haya mafuta ziko kwenye hatua nzuri kila sehemu ambayo nimeenda linakopita bomba hii kazi inaendelea vizuri.
Aidha alisema kuwa kwa upande wa Uganda tayari jumla ya pampu 6 zitakazotumika kuvuta mafuta kutoka ardhini zimeshafungwa.
"Kule Uganda tayari wameshafunga pampu 6 za kuvuta mafuta kutoka ardhini kwa maana hiyo mradi huu kwa kutathmini unakwenda vizuri , nawapongeza sana Kambi hii ya chongoleani kwa kazi na juhudi ambazo wanaendelea kuzifanya katika kuhakikisha matakwa ya Serikali yetu yanafikiwa", aliongeza Balozi Kisesa.
Awali akizungumza msimamizi wa Kambi ya Chongoleani Reni Bezian kupitia kampuni ya DOCG amesema kuwa tayari kufikia sasa wameshafikia asilimia 20 ya utekelezaji wa mradi kwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mapima manne yaliyopo kwenye hatua ya awali ambayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhia mafuta million nne lengo lao likiwa ni kukamilisha kabla ya Kambi zote zinqzopitiwa na mradi huo.
" Mpaka sasa tumefikia asilimia 20 kwa ujenzi wa miundombinu inayopaswa kuwepo hapa Chongoleani na asilimia 60 kwa upande wa mapipa ya kuhifadhia mafuta tayari tumeshaanza hatua ya awali lengo letu ni kukamilisha kwa wakati na sasa tunawekeza nguvu zetu zote kuhakikisha tunakamilisha lengo la mradi mpaka 2026", alisema Bezian.
Aliongeza kuwa wanaendelea kutekeleza matakwa ya maktaba ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira pamoja na kutoka ajira kwa wazawa ambapo mpaka sasa katika Kambi hiyo Kuna wafanyakazi 1011 zaidi ya 800 wakiwa ni wazawa wakiwemo wenye ujuzi 573, wasio na ujuzi 284.