Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI SHINYANGA WADAKA WATUHUMIWA 55, MALI MBALIMBALI ZA WIZI


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani akizungumza na waandishi wa habari - Picha na MALUNDE
Katika kuhakikisha Usalama waa raia na mali zao, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Jamii pamoja na vyombo vingine vya ulinzi katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kufanya doria, misako, operesheni na kutoa elimu kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 25,2024 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani amesema  kuanzia Agosti 22, 2024 mpaka Septemba 24, 2024 Jeshi la Polisi Mkoa wa  Shinyanga  limefanikiwa kukamata watuhumiwa 55 pamoja na vielelezo mbalimbali.

Amevitaja vielelezo hivyo kuwa ni mafuta ya petroli lita 55, mitungi 05 ya gesi, tairi 02 za gari, Pikipiki 05, simu 09, Redio 02, Boksi 10 za pombe aina ya roboti, Seti ya CCTV CAMERA, TV 03, Jenereta 01, pombe ya moshi lita 10, mtambo 01 wa kutengeneza pombe ya moshi, Laptop 01 na vifaa mbalimbali vya kupiga ramli chonganishi.


Kwa upande wa mafanikio ya kesi mahakamani, amesema jumla ya kesi 19 zimepata mafanikio ambapo kesi 01 ya kulawiti mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha maisha jela, kesi 02 kubaka washtakiwa 02 walihukumiwa miaka 30 jela, kesi 02 unyang'anyi wa kutumia silaha washtakiwa 02 walihukumiwa miaka 29 na miezi 05 jela, kesi 02 za kula njama washtakiwa 07 walihukumiwa miaka 13 jela kesi 01 kupatikana na madawa ya kulevya aina ya bhangi mshtakiwa alihukumiwa miaka 02 jela.


Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kesi 01 ya gari kumgonga mpanda baskeli na kusababisha kifo mshtakiwa amefungiwa leseni kwa kipindi cha miaka mitatu, kesi 05 za kuingia kwa jinai washtakiwa 06 walihukumiwa miaka 03 jela, kesi 01 wizi wa mtoto mshtakiwa alihukumiwa mwaka mmoja na nusu jela, kesi 01 kupatikana na noti bandia mshtakiwa alihukumiwa mwaka 01 jela na kesi 03 za wizi washtakiwa 03 walihukumiwa miezi miwili mpaka sita jela. 

"Lakini pia Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kupitia kikosi cha Usalama barabarani limefanikiwa kukamata jumla ya makosa 5,048 kwa mchanganuo ufuatao;- makosa ya magari ni 3,460 na makosa ya bajaji na pikipiki ni 1,588 wahusika waliwajibishwa kwa kulipa faini za papo kwa hapo",amesema Kamanda Mgani.

Akizungumzia kuhusu utoaji wa elimu, amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kufanya jumla ya mikutano 41 ya uelimishaji kwa jamii ikiwemo shuleni, mikutano ya hadhara na vikundi 34 vya ulinzi shirikishi vimepatiwa elimu ya ukamataji salama wa wahalifu kwa kuzingatia haki za binadamu pia waendesha pikipiki maarufu bodaboda wameelimishwa kuzingatia taaluma yao waliyoipata pindi wawapo vyuoni katika uendeshaji salama na kuzingatia Sheria za Usalama barabarani wakati wanapotumia vyombo vya moto.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaishukuru jamii kwa kuendelea kupokea elimu inayotolewa kwa ushirikiano madhubuti katika kuhakikisha Usalama wa Mkoa wa Shinyanga unakuwa shwari sambamba na kupokea elimu inayotolewa, pia linatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutii na kufuata Sheria, taratibu na kanuni za nchi',ameongeza.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com