DR. MLACHA : WANANCHI TEMBELEENI VITUO VYA AFYA MPIME HOMA YA INI

Na George Mganga, SHINYANGA RRH

WANANCHI wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na maeneo jirani wametakiwa kutembelea vituo vya afya kwa ajili ya kupima afya zao hususani Homa ya Ini, ili kuepukana na changamoto za kiafya ikiwemo kansa ya ini na kifo.

Hayo yamesemwa Septemba 25, 2024 na Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha, wakati akitoa elimu ya ugonjwa huo kwa watumishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Mlacha ameeleza maambukizi ya ugonjwa huo yanasababishwa na virusi ya Homa ya Ini, ikichagizwa zaidi na ngono zembe, kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pia kwa mfumo wa majimaji (kukumbatiana na mtu mwenye jasho).

“Tujitahidi kufanya vipimo ili kujua hali ya afya zetu, huu ugonjwa namna unavyoambukiza ni sawa na virusi vya UKIMWI.

“Ukishapima na ukagundulika uko salama utapata chanjo na utaishi salama”, amesema Dkt. Mlacha.

Aidha, Mlacha amesema takwimu zinaeleza kuwa utafiti uliofanyika, zaidi ya asilimia 95 ya waliopata chanjo ya Homa ya Ini hawajafanikiwa kupata maambukizi ya ugonjwa huo ambao umekuwa na athari kubwa ikiwemo Kansa ya Homa ya Ini.

Ameainisha baadhi ya athari ambazo zinaweza kumpata mtu mwenye ugonjwa huo ukiachilia Kansa ya Ini, ni ini kutofanya kazi yake, lakini vilevile inaweza pelekea mtu akapoteza uhai.

Ili kujikinga, Mlacha amewasihi wananchi waepukane na ngono zembe, kuwa na wapenzi wengi, kufanya ngono salama na muhimu zaidi kupata chanjo mapema kwa ajili ya kuepukana na homa hiyo.

Mlacha pi ameeleza rika ambalo linapaswa kupata chanjo mapema zaidi, na ambalo lina hatari kubwa ya kupata maambukizi, ni kundi la vijana kuanzia umri wa miaka 14 na kuendelea.

Halikadhalika, ili kutokomeza na kuzuia maambukizi ya Homa ya Ini, Mlacha anawapa wito wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine kuhakikisha wanafika kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupima.

Amehitimisha kwa kueleza ugonjwa wa Homa ya Ini hauna TIBA, bali una dawa zinazosaidia kufubaza makali ya virusi hivyo ili visisababishe athari zaidi kiafya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post