Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MACHA AFUNGUA MAADHIMISHO WIKI YA VIZIWI DUNIANI KITAIFA SHINYANGA..AZIPA JUKUMU HALMASHAURI MKAZO LUGHA YA ALAMA

 

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,ameziagiza halmashauri za mkoa huo,kwamba kila mwaka wa fedha watenge bajeti ili kuwapeleka kozi maafisa habari,mawasiliano na uhusiano wasomee kozi ya lugha ya alama,ili wasaidie  viziwi kupata huduma kwa kutoa tafsiri.

Amebainisha hayo leo Septemba 25,2024 wakati akifungua Rasmi maadhimisho ya kumi na moja ya wiki ya viziwi duniani, ambayo kitaifa yataadhimishwa mkoani Shinyanga Septemba 28, katika viwanja vya Sabasaba Manispaa ya Shinyanga.

Macha amesema kutokana na kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema “Ungana kutetea haki za lugha ya alama,” kwamba watu viziwi hawana tofauti na wengine, bali hutofautishwa na lugha ya mawasiliano tu,na hivyo kuagiza halmashauri zote mkoani humo, kutenga bajeti kila mwaka,ili kuwapeleka kozi maafisa habari,mawasiliano na uhusiano kusomea lugha ya alama.
“Serikali inatambua umuhimu wa kukuza lugha ya alama,ndiyo maana kuna vyuo vinavyofundisha lugha hizo, na mimi naagiza halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga, kutenga bajeti kila mwaka ili kuwapeleka kwenye kozi maafisa habari,mawasiliano na uhusiano kusomea lugha hizi za alama, ili kusaidia kutoa huduma stahiki kwa watu viziwi, kwa wao kutoa tafsiri,”amesema Macha.

Aidha, amesisitiza pia kwenye taasisi zote za serikali pamoja na binfasi, wajitahidi pia kuwa na Wakalimani wa lugha ya alama, ili kusaidia kutoa huduma stahiki kwa watu viziwi wanapofika kwenye taasisi hizo.
Macha amesisitiza pia ufuatwaji wa sheria ya ajira kwenye taasisi za serikali na binafsi, ambayo inasema asilimia 3 ya ajira waajiriwe watu wenye ulemavu,huku akiomba kupatiwa takwimu sahihi za watu wenye ulemavu na ujuzi wao,ili nafasi zikitoka za ajira halmashauri waone namna ya kuwa ajiri kila mmoja na ujuzi wake.

Amezungumzia pia suala la uchaguzi wa Serikali za mitaa, na kuwataka watu wenye ulemavu mbalimbali wajitokeze kuwania nafasi za uongozi,pamoja na kushiriki kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo na kutatua shida zao.
Amesema watu hao wenye ulemavu na wao wanasifa ya kuwa viongozi na tena ni viongozi wazuri, ndiyo maana hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa wakiwapatia nafasi za uongozi katika serikali yake, na kuwasihi wananchi kwamba watu hao wakiomba nafasi za uongozi wawapatie fursa.

Katika hatua nyingine Macha, amewaomba wazazi wasiwafiche ndani watoto wenye ulemavu,bali wawapatie elimu sawa na watoto wengine, na kwamba serikali imeboresha mazingira na miundombinu rafiki ya watoto hao kusoma.
Mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Selina Mremba, amesema lugha ya alama ndiyo chombo cha mawasiliano kwa watu viziwi, na kusisitiza suala la kuwepo kwa Wakalimani wa lugha hiyo kwenye taasisi zote binafsi na Serikali.

Ameiomba pia serikali,kuweka mazingira rafiki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ili watu viziwi na wao wapate kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo.
Mwakilishi shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) Ghati Horombe,amesema ili taifa lipate kufikia maendeleo endelevu, lazima ujumuishwaji wa makundi yote yashirikishwe,na kwamba katika maadhimisho hayo watatoa pia mafunzo kwa watu viziwi ya uchumi wa kidigital.

Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi wilayani Kahama Zawadi Masoud, akisoma risala ya Chama cha Viziwi mkoa wa Shinyanga, ameomba kuwepo na Wakalimani wa lugha ya alama kwenye taasisi za serikali na binafsi, ikiwamo Polisi, Mahakama na Hospitali, ili kusaidia upatikanaji wa mawasiliano pale wanapofika kupata huduma.
Ameomba pia kuwapo na utengwaji wa bajeti kwa halmashauri ili kusaidia watu viziwi kushiriki kwenye maadhimisho ya kitaifa, pamoja na kushirikishwa kwenye vikao mbalimbali vya maamuzi.

Kilele cha maadhimisho ya kumi na moja ya viziwi dunia, yatafanyika Septemba 28,2024 na kitaifa yatafanyikia mkoani Shinyanga.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza wakati akizundua maadhimisho ya wiki ya viziwi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamdun akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya viziwi.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya viziwi.
Mwakilishi wa UNDP Ghati Horombe akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya viziwi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Selina Mremba, akitoa salamu.
Afisa ustawi Mwandamizi Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi,vijana,ajira na watu wenye ulemavu Gerold Komba akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya viziwi.
Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi wilayani Kahama Zawadi Masoud akisoma risala.
Ufunguzi wa maadhimisho ya kumi na moja ya wiki ya viziwi yakiendelea .
Picha za pamoja zikipigwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com