Mwenyekiti wa kamati ya shule , Bw. Abraham Dauson
NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE.
KATA ya Bwilingu katika halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani imepania kuongeza shule kutokana na mahitaji ya jamii husika.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Bwilingu, Mh. Nasser Karama alipokuwa akihutubia katika mahafali ya kwanza ya darasa la saba katika shule ya msingi Ridhiwani Kikwete mjini hapa jana.
Mh. Nasser amesema bado jamii ya kata yake inahitaji huduma zaidi katika elimu, ila katika hatua inayofuata watajenga shule ya sekondari eneo la Chalinze Mzee na shule nyingine ya msingi eneo la Koo katika kata ya Bwilingu.
Diwani Nasser amesema kwa kufikia hatua hiyo kata ya Bwilingu itakuwa na shule 13 za msingi na shule 5 za sekondari.
Akijibu risala ya shule hiyo ,mgeni rasmi meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Chalinze Bw. Boniphace Shija amesema benki inakwenda kujenga jiko kwaajili ya huduma shuleni huku mahitaji mengine ikiwa pamoja na mashine ya fotokopi na ujenzi wa nyumba za walimu utasubiri hadi taasisi yake itakapopata uwezo.
"Ombi la ujenzi wa jiko la shule tunakwenda kushughulika nalo, ila huduma zingine zinahitaji muda na bajeti zaidi",alisema mgeni rasmi huyo.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuzumgumza, Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Bw. Abraham Dauson aliipongeza benki hiyo kwa kuipa shule meza na viti 50 bila kusahau kuwasaidia mfumo wa umeme shuleni hapo kwa siku za hivi karibuni.
Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Gema Kinyange amewaambia wazazi kuwa wajiandae kupeleka watoto wao kidato cha kwanza mwakani, kwani ana imani kubwa na kazi iliyofanywa na walimu wake katika ufundishaji.
Jumla ya wanafunzi 96 wamehitimu elimu ya msingi katika shule hiyo kwa mwaka 2024.
Social Plugin