DARAJA HURUI KUWA KITOVU CHA UCHUMI KONDOA




NA DOTTO KWILASA, DODOMA

Kazi ya Ujenzi wa Taifa si lelemama hata kidogo, inahitaji hasa kujitoa muhanga kwelikweli kutokana na vikwazo vingi ambavyo ili kuvishinda inabidi uwe na moyo wa kishujaa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wake Dk. Samia Suluhu Hassan inatekeleza kazi hii kwa wivu mkubwa kwa kuzingatia uzalendo na kujitoa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na mazingira mazuri ya kuishi.

Sote ni mashahidi, kishindo cha Mguu kwa mguu, hatua kwa hatua, Wilaya kwa Wilaya hadi Mikoa kwa Mikoa imekuwa ni Utamaduni wake kutekeleza kwa vitendo maendeleo ya miradi ya kimkakati inayowasaidia wananchi ikiwemo ya maji,barabara na umeme.

Yote haya yanajidhihirisha Wilayani Kondoa
ambako Serikali imejenga ujenzi uliovunja mwiko wa kihistoria wa Daraja la mto Hurui lililopo kata ya Kikore Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma lenye thamani ya shilingi bilioni 1.5.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 30 linatajwa kuwa kiungo muhimu kati ya wilaya ya Babati na kondoa ambapo usanifu wake umefanywa na wahandisi wazawa chini ya Kitengo cha "TARURA na ujenzi wake ukiwa umefanywa na Kampuni ya uwekezaji ya Mkandarasi Madata na Utekelezaji wake umefikia asilimia 95 kukamilika huku daraja likiwa na uwezo wa kubeba magari uzito wa tani 70 na litadumu kwa zaidi ya miaka 100.

Wananchi wa kijiji cha Hurui kata ya Kikore Wilayani hapo wanasema ujenzi wa daraja hilo la kisasa lenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 linalotarajiwa kukamilika mwisho mwa mwezi Disemba 2024 litatatua kero ya muda ya mrefu ya kutumia daraja la kamba lililojengwa na wakoloni kuvuka mto na kusaidia kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii .

Saleh Shaban anaeleza kuwa kabla ya daraja hilo kukamilika watoto walishindwa kufika shule kwa wakati na wakati mwingine kwenye kipindi cha mvua walishindwa kabisa kuhudhuria masomo huku wakazi wa Kijiji hicho kushindwa kuuza mazao yao kutokana na kukosekana kwa miundombinu hiyo.

Anaeleza kuwa mradi wa Daraja la Hurui ni mojawapo ya miradi muhimu katika eneo hilo kwa kuwa linaunganisha barabara kuu na maeneo ya ndani, likilenga kuboresha usafiri wa watu na mizigo kati ya Kondoa na maeneo mengine.

"Tuna furaha sana kwani daraja hili linaenda kurahisishaji Usafiri na kupunguza muda na gharama za usafiri, na hivyo kuimarisha uchumi wa eneo hilo pamoja na kuongeza Fursa za Biashara zitakazo chochea uchumi na kuongeza ajira na kipato kwa jamii," amefafanua mwananchi huyo wa Hurui Kondoa.
Naye Mariam Idd anasema daraja hilo litaongeza usalama kwa watoto na kusaidia kupunguza ajali ambazo zilitokana na Daraja bovu la kamba lilikuwepo mwanzo na kuchangia katika kuboresha huduma za kijamii kama elimu na afya, kwani watu wanapata urahisi wa kufikia huduma hizo.

Ili kuweka uhifadhi wa daraja hilo,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango
Agosti 21 ,2024 anapiga hodi Wilayani hapa ambapo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja hilo ambalo limekamilika kwa asilimia 90 huku macho na masikio yote yakiwa yanasubiri uzinduzi wake utakaofanywa na Rais Samia Suluh Hassan.

Makamo huyo wa Rais akiwa mwenye dhamana ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira anawahimiza wananchi wa kata ya Kikore na watumiaji wa daraja hilo kutunza miundombinu iliyojengwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwaagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) kufanya ukarabati wa Barabara ya Ntundwa – Hurui ya Wilayani Kondoa ili kuwarahisishisa wananchi shughuli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji mazao huku amkiagiza kupandwa miti maeneo yote ya pemebezoni mwa mto hurui ili kuokoa daraja hilo lisiharibike kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Mbali na hayo aliwapongeza wananchi hao kwa kupata mradi wa daraja hilo ambalo litawaondolea changamoto waliyopata ya kukosa daraja tangu mwaka 2019 lilipoharibiwa na maji daraja la awali na kuwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali itaendelea kuwafikishia wananchi huduma muhimu ikiwemo miundombinu ya umeme.

Akiwa kata ya Kikore ameagiza kukamilishwa kwa mradi wa maji unaotekelezwa katika kata hiyo ifikapo tarehe 30 mwezi Oktoba 2024.

"Naiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini kushughulikia changamoto iliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Hurui kuhusu ardhi ya Kijiji inayodaiwa kuuzwa kwa mwekezaji bila kufuata utaratibu, "alisema

Suala hilo linamuibua Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Dkt. Festo Dugange ambaye anaeleza kuwa daraja hilo limejengwa ikiwa ni maelekezo ya Mhe. Rais Dr. samia Suluhu Hasan katika kuhakikisha vijiji vyote vinapitika katika kipindi chote.
Dugange anaeleza kuwa mbali na daraja hilo Serikali inaendelea na mpango wake wa kuzipandisha hadhi barabara kutoka udongo kuwa changarawe lakini kutoka changarawe au udongo na kuwa barabara za lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii.

"Tunahudumia zaidi ya Klm. 144,000 ya mtandao wa barabara lakini zaidi ya Km. 100,000 ni barabara za udongo, hizi ndio zina changamoto kubwa msimu wa mvua kwani maeneo mengi yanakuwa hayapitiki na kutokea taharuki ndio sababu tunajitahidi kadri rasilimali fedha tunazopata kuhakikisha kwamba tunaondoa vikwazo vyote ili barabara ziweze kupitika misimu yote ya mvua", aameeleza

Naye Mtendajj Mkuu wa wakala ya barabara mijini na Vijijini (TARURA)Mhandisi Victor Seff amesema Mradi huo umehusisha uboreshaji wa kilometa 8 za barabara kwa kiwango cha changarawe na umegharamiwa na Serikali kupitia tozo ya mafuta ya shilingi 100.

Anasema kuwa kipaumbele cha kwanza ni matengenezo ya miundombinu ya barabara ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika, ikiwa ni kuendelea na matengenezo hata pale barabara na madaraja yanapokamilika ili miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.

Anaeleza kuwa kipaumbele kingine ni kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili ziweze kupitika katika misimu yote ya mvua, mojawapo ya kazi ya kuondoa vikwazo ni pamoja na kujenga barabara kwa kutumia zege, kuweka makalavati na vivuko maeneo yote korofi ili hadi kufikia mwaka 2025/26 asilimia 85 ya mtandao wa barabara za Wilaya uweze kupitika nyakati zote.

"Mtandao wetu una zaidi ya Km. 144,000 lakini rasilimali fedha tunazopata bado ni kidogo, hivyo tunajitahidi kadri tunavyopata rasilimali fedha tunaondoa vikwazo ili barabara zetu ziweze kupitika nyakati zote", alisema Mhandisi Seff.

Vile vile anaongeza kusema kuwa Wakala unatumia teknolojia mbadala pamoja na malighafi za ujenzi zinazopatikana maeneo ya kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post