DAWASA KUSHIRIKIANA NA JAMII KUBORESHA MIFUMO USAFI WA MAZINGIRA BUGURUNI
الجمعة, سبتمبر 06, 2024
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imepanga kuanza mkakati jumuishi na wakazi wa Buguruni kisiwani, katika Wilaya ya Ilala katika utunzaji wa miundombinu ya Usafi wa Mazingira ili kumaliza changamoto ya utiririshaji majitaka katika makazi ya watu.
Akizungumzia alipotembelea na kukagua mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka katika Makazi uliotekelezwa katika eneo hilo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire ameeleza kuwa jamii inaposhirikishwa katika usimamizi na uendeshaji wa miradi ya kijamii kama hii huleta mafanikio makubwa.
"Kila penye mafanikio huja na changamoto, changamoto ya mradi huu tumeitambua na wakati tunaendelea na mipango mikubwa ya uboreshaji tumeona tuanze kwa kushirikisha jamii husika kwanza kwa kuwapatia elimu ya matumizi sahihi ya mfumo lakini pili uendeshaji wa mradi ni lazima jamii hii ihusike katika uendeshaji na utunzaji wa mradi huu"ameeleza Mhandisi Bwire.
Mhandisi Bwire ameongeza kuwa kwa kuwatumia Wananchi wazawa wa eneo husika katika utunzaji na uendeshaji wa mradi ni dhahiri kutatoa chachu ya elimu kwa jamii m juu ya matumizi sahihi ya mfumo wa uondoshaji majitaka katika makazi.
Nae Diwani wa Kata ya Buguruni Mheshimiwa Bussolo Pazi amemshukuru Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA kwa kufika eneo la Buguruni kisiwani na kujionea changamoto inayowakabili akiamini kuwa changamoto ya uchafuzi wa Mazingira inakwenda kumalizika katika Kata hiyo.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amefanya ziara ya kukagua mfumo rahisi wa uondoshaji Majitaka eneo la Buguruni kisiwani kufuatia maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Edward Mpogolo aliyotoa mapema wiki hii kumtaka afike na kuangalia namna bora ya DAWASA kuimarisha mifumo hiyo ili kutunza afya za Wakazi.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin