DAWASA MBIONI KUKAMILISHA MRADI WA MAJI WSSP II TEMEKE

 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ipo mbioni kukamilisha mradi wa uboreshaji huduma ya Majisafi awamu ya pili (WSSP II) katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa wakazi wa mtaa wa Mwanamtoti katika kata ya Kijichi, Wilaya ya Temeke utakaonufaisha wakazi takribani 13,000.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa DAWASA Mbagala Alex Mwanja amesema eneo la Mwanamtoti limekuwa na changamoto ya huduma ya maji kwa kipindi kirefu na kupelekea Wananchi kutumia huduma ya maji ya visima na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu utakuwa suluhisho la kudumu kwa wakazi waishio eneo hilo.

"Mradi huu ulianza mnamo mwaka 2022 na unategemea kukamilika Oktoba 2024, utekelezaji wake umefikia asilimia 99 na baadhi ya wananchi wameanza kupata huduma ya Majisafi kwa baadhi ya maeneo kama vile Mwanamtoti, Butiama Mwembe Bamia, Kisewe na Dovya” ameeleza Mhandisi Mwanja.

Mhandisi Mwanja ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi kutanufaisha wananchi zaidi ya 13,500 wa eneo la Mwanamtoti waliodumu na changamoto ya ukosefu wa huduma kwa takribani miaka 10.

Mtendaji wa mtaa wa Mwanamtoti ndugu Mohamed Mussa amesema kuwa changamoto ya maji katika mtaa huo ilikuwa ni kubwa sana kutokana na kufuata maji kwa umbali mrefu na kuyapata kwa gharama kubwa huku wakiwa hawana uhakika na ubora wake.

"Nipenda kuwashukuru sana Serikali ya awamu ya Sita kwa kusimamia vyema kukamilishwa kwa mradi huu, pia DAWASA usimamizi maana wametusaidia sana kwa sababu awali huduma ya maji ilikuwa inafuatwa mbali na gharama kubwa, lakini pia ubora wa maji hayo haukuwa unajulikana hivyo kuwa hatarishi kwa afya zetu" ameeleza ndugu Mussa

Bi. Fatuma Bakari mkazi wa Mwanamtoti ameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa iliyofanywa kuhakikisha uhaba wa maji uliodumu kwa kipindi cha miaka 10 unafika kikomo.

Mradi wa uboreshaji huduma ya Majisafi awamu ya pili (WSSPII) umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 10.5 na unaenda kuwa suluhisho la kudumu la uboreshaji wa huduma ya Majisafi hususani Wilaya ya Temeke katika Kata tatu za Kijichi, Mianzini na Chamazi zenye jumla ya mitaa 9 ya Mwanamtoti, Butiama, Mponda, Mianzini, Machinjioni, Mwembe bamia, Kisewe, Magengeni, na Dovya.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post