Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Septemba 23, 2024 amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kikao na Ujumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Vietnam ukiongozwa na Mhe. Phan Dinh Trac kilichofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Biteko ameeleza kuwa Tanzania na Vietnam zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na zinaendelea kuimarisha uhusiano huo katika nyanja za diplomasia, siasa na uchumi.
Aidha, ameipongeza Vietnam kwa kufanya uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo katika Kampuni ya Simu za Halotel na kusema kuwa nchi hizo zinahitaji kuongeza kiwango cha biashara kati yake ambapo kiwango cha uwekezaji kwa sasa ni dola za kimarekani milioni 300.
Kwa upande wake, Mhe. Trac ameipongeza Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuvutia uwekezaji, kuboresha huduma za afya, sambamba na kupiga vita vitendo vya rushwa.
Ameongeza kuwa, kufuatia jitihada hizo kiwango cha ukuaji uchumi kwa mwaka nchini Tanzania kimefikia asilimia 6.5 na kuwa Tanzania ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya Afrika na dunia kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Trac ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania uliodumu kwa takribani miaka 60.
Pia, ameiomba Tanzania kuwa kiunganishi kati ya Vietnam na Umoja wa Afrika katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Social Plugin