NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko amesema kampuni ya Oryx Gas imekuwa ikitoa ushirikiano kwa Serikali na wamekuwa wakishiriki katika matukio mblimbali ya kugawa mitungi ya gesi na majiko yake kwa wananchi sambamba na utoaji mafunzo ya matumizi salama ya nishati safi ya kupikia.
Ameyasema hayo leo Septemba 8,2024 wakati wa Hafla ya Azimio la Kizimkazi iliyolenga kuunga mkono jitihada za Rais, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya Kupikia ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Pika Kijanja inayoendeshwa na kituo cha redio cha Bongo Fm na Televisheni ya TBC.
Aidha ametoa wito kwa Watanzania kuokoa maisha yao kwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ambayo itawaepusha na madhara yanayotokana na Nishati isiyo safi ikiwemo athari katika mfumo wa upumuaji.
Dkt. Biteko amesema, Rais Samia licha ya kuwa kinara wa Afrika kwenye kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia, pia amedhamiria kuwaondoa kina Mama na Baba Lishe wa Tanzania katika matumizi ya Nishati isiyo safi na pia kuboresha hali zao kwa kutumia Nishati safi ya Kupiki ambapo ametoa mitungi 2,000 kwa kundi hilo kama njia ya uhamasishaji wa nishati hiyo.
"Nipende kumpongeza sana Mhe Rais kwa kuibeba ajenda hii ya Nishati safi ya Kupikia na kwa maono aliyonayo, nitoe agizo kwa Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha Wizara inashirikisha wadau kwenye kampeni hii ili iweze kufanyika kwa ufanisi na hivyo kumuunga mkono Mhe. Rais." Amesema Dkt. Biteko.
Akitoa takwimu za hali ilivyo kwa sasa, Dkt. Biteko amesema watu Bilioni 5.8 duniani ndio wanatumia Nishati Safi huku Bilioni 2.4 wakitumia Nishati isiyo safi ambapo Afrika Pekee ina watu milioni 933 wanaotumia Nishati isiyo safi na hivyo kuwataka wadau kuuganisha nguvu kuunga mkono matumizi ya Nishati iliyo safi.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Baba na Mama Lishe nchini na ndio mana kwenye hafla hiyo ya Azimio la Kizimkazi wamealikwa ili kuwahamasisha kuondokana na matumizi ya Nishati chafu na hivyo kuboresha mazingira yao ya ufanyaji kazi kwa kuwapatia Mitungi ya gesi kama Nishati mojawapo iliyo safi.
Amesema kimsingi muktadha wa Mhe Rais kama Kinara wa Nishati safi ya Kupikia Afrika ni utekelezaji pia wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoelekeza Watanzania kupatiwa Nishati Safi ya Kupikia kwa wakati na kwa gharama nafuu na ndio maana mitungi takriban 450,000 iliamuliwa iuzwe bei ya ruzuku ili kuwafikia wananchi.
Akizungumza wakati akitoa salamu za Oryx kwa Serikali pamoja na wageni waalikwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Benoit Araman amesema Oryx Gas Tanzania inafanya kazi bila kikomo kila siku ili kutekeleza maono ya Rais Samia ya kwamba asilimia 80 ya Watanzania ipate nishati ssafi ifikapo 2034.
“Mpango huu utafanikiwa tu ikiwa tumejitolea kutumia nishati safi ya kupikia kila siku.Leo hii katika muendelezo ule ule wa kuunga mkono jitihada za Rais Samia tunakabidhi mitungi ya gesi yq Oryx 1000 kwa Mama na Baba Lishe ambao wameungana nasi katika hafla hii ya Pika Kijanja.”
Pia amemshukuru Waziri wa Nishati, Dk Biteko na Naibu Waziri Kapinga kwa kuwashirikisha ambapo mbali ya kutoa mitungi ya gesi wametoa mafunzo yq matumizi salama ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumzia faida na kutumia nishati safi ya kupikia ,Benoit amesema kiafya nishati safi inasaidia kuokoa maisha kwani kumekuwa na vifo vinavyotokana na magonjwa ya upuamuji yayanayosababishwa na matumizi yq nishati chafu.
“ Nchini Tanzania, wananchi 33,000 wanakufa kila mwaka kutokana na kuvuta pumzi ya moshi na chembe chembe zinazotokana na mkaa na kuni. Kupika na Oryx LPG kutasaidia kumaliza changamoto hiyo ya kiafya lakini kwa mazingira kupika kwa nishati safi huzuia ukataji miti na hivyo kulinda mazingira”
Ameongeza kuwa kupika kwa nishati safi husaidia kuzuia wanawake kufanya kazi ngumu ya kutumia muda mwingi kukusanya kuni kutoka msituni.Pia kupika kwa nishati safi husaidia kuwaweka wanawake katika hali ya usalama kwani porini kumekuwa na hatari nyingi.
Social Plugin