DKT. YONAZI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA UONGOZI WA PSARP


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza na wageni kutoka Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (Protective Security & Attack Response Programme – PSARP) chini ya Ubalozi wa Uingereza kuhusu uwezekano wa kuandaa Mpango wa Kuimarisha Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Maafa walipomtembelea Ofisini kwake tarehe 12 Septemba, 2024 Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (Katikati) akiwa katika picha ya Pamoja na ujumbe kutoka Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (PSARP) wakiongozwa na Mratibu wa Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (PSARP) - Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara Bw. John Spencer (kushoto kwake)na kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya utafiti wa maafa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi.
Mratibu wa Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (PSARP) - Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara Bw. John Spencer akizungumza jambo wakati wa kikao na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi walipomtembelea Ofisini kwake Jijini Dodoma.

NA. MWANDISHI WETU

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na Mratibu wa Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (Protective Security & Attack Response Programme – PSARP) chini ya Ubalozi wa Uingereza kuhusu uwezekano wa kuandaa Mpango wa Kuimarisha Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Maafa.

Amekutana nao mwishoni mwa wiki walipomtembelea Ofisi kwake Jijini Dodoma, na kueleza kuwa PSARP inalengo la kuimarisha uwezo wa Wataalam katika kukabiliana na maafa nchini.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Yonazi ameshukuru uongozi huo kwa kumtembelea na kutumia fursa hiyo kujadili majukumu ya msingi ya Ofisi yake ya kuratibu Shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na uratibu wa masuala ya maafa nchini ambalo ndilo eneo walilolenga kuzungumza na kuona namna bora ya kushirikiana na Serikali.

Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (PSARP) - Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara Bw. John Spencer ameipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kutekeleza majukumu yake ikiwemo suala la menejimenti ya maafa huku akielea lengo la Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi ambao umejikita katika kuimarisha utendaji wa polisi katika operesheni za dharura na kuona fursa katika kushirikiana na nchi ya Tanzania ili kuimarisha utendaji wa pamoja wa taasisi zinazohusika na kukabiliana na maafa.

Aliongezea kuwa wapo tayari kushirikiana ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha uwezo wa kukabiliana na maafa kwa kuwajengea uwezo wataalam wa maafa katika eneo la mfumo jumuishi wa utendaji wa pamoja wakati wa dharura.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post