FAMILIA YA MAREHEMU KING MAJUTO YAOMBA UMEME

Na Hadija Bagasha Tanga, 

Familia ya aliyekuwa mwigizaji maarufu hapa nchini Alhaji Amri Athumani maarufu kama 'King Majuto'   imeiomba Serikali kuwafikishia  huduma ya umeme katika makazi aliyokuwa akiishi msanii huyo ambapo aliacha Msikiti pamoja na Madrasa  vinavyotumika hadi sasa na jamii iliyopo.

Akizungumza kwa niaba ya familia mtoto wa tatu wa 'King Majuto'  Haruna Athumani  amesema kuwa bado jamii inaendelea kumuenzi na kumkumbuka msanii huyo kutokana na huduma alizozianzisha  ikiwemo Msikiti, Madrasa pamoja na Kisima ambavyo vinawanufaisha wananchi waliopo karibu yao.

"Tunashukuru sana Mkuu wa wilaya kututembelea na kutupa sadaka yake kwaajili ya Mzee wetu lakini pia niwaombe wadau wengine na viongozi wa Serikali kushiriki kwa njia moja ama nyingine kusaidia familia hii hapa tuna shida ya umeme  kwa sababu eneo hili mzee wetu alilianzisha yeye lakini sasa hivi kuna jamii ambayo ipo kwahiyo eneo hili kwa sasa Lina shida ya maji na umeme tukipata hivyo vitu tunashukuru sana kwasababu vitasaidia jamii iliyopo kwa sasa" alisema Haruna.

Familia imetoa ombi hilo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Tanga Japhari Kubecha ambaye alitembelea na kudhuru kaburi la msanii huyo na kushiriki dua maalum ya kumwombea pamoja na familiya  yake katika Mtaa wa Kiruku kata ya Mabokweni halmashauri ya Jiji la Tanga.

Kufwatia ombi hilo la familia  Mkuu wa wilaya hiyo Japhari Kubecha amemwagiza kaimu katibu  tawala Mussa Machunda kuwasiliana na ofisi ya Shirika la umeme Tanzania 'Tanesco'  kuangalia uwezekano wa kumaliza changamoto  hiyo.

Amesema Serikali ya wilaya ya Tanga itaendelea kumtambua mchango wa msanii huyo ambaye amekuwa kielelezo kwa jamii kupitia kazi zake za sanaa alizozifanya kuelimisha  na kuburudisha katika nyanja mbalimbali.

"Ki ukweli Mzee Majuto' alikuwa ni msanii ambaye alimtumia sanaa yake kutuunganisha nchi yetu pamoja na kuikuza Lugha yetu ya Kiswahili, kila alipopata nafasi aliubeba utaifa maadili katika sanaa yake alihakikisha analinda heshima na hadhi ya maadili ya mtanzania tofauti na uigizaji wa sasa hivi "

"Kama Serikali sisi tunaahidi kuendelea kutoka mchango wetu kwa familiya ili kuenzi  kazi zake lakini kumtambua kama miongoni mwa wazee maarufu ambao kwa nafasi yake aliitangaza wilaya yetu ya Tanga  kupitia kazi zake, uvaaji wake  hii inaonyesha aliubeba uhalisia wa Tanga na desturi zake" alisema Kubecha.

Msanii King Majuto' mbaye alizaliwa  mwaka 1Augost 1948 Mkoani Tanga  na kufariki 8Augost 2018 aliwahi kutamba na filamu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Mama ntilie, Sio sawa, Rent hause ,Mrithi wangu , Ndoa ya utata, Dala Dala, Nimekuchoka na nyinginezo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post