Mtoto wa aliyekuwa Kiongozi wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Marehemu Ali Mohamed Kibao,Maryam Ali Kibao akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni(kulia), baada ya kutembelewa na kufarijiwa wakati wa msiba wa baba yake aliezikwa jijini Tanga. Wapili kulia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Abdulrahman Shiloow.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu,Tanga
Familia ya Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA),Marehemu Ali Mohamed Kibao aliyezikwa juzi jijini Tanga wameiomba serikali kuharakisha uchunguzi wa kifo cha baba yao ambae mwili wake ulipatikana maeneo ya Ununio jijini Dar es Salaam akiwa ameuawa baada ya kutekwa na watu wasiojulikana Ijumaa ya Septemba 6, 2024 katika maeneo ya Tegeta karibu na Jengo la Kibo Complex.
Wametoa ombi hilo mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni baada ya Waziri huyo kufika nyumbani kwa marehemu jijini Tanga kutoa salamu za pole kwa niaba ya serikali ambapo pia aliwasilisha rambirambi ya kiasi cha shilingi milioni tano kwa niaba ya serikali.
Akizungumza mbele ya Waziri Masauni kwa niaba ya familia mtoto wa marehemu Ali Mohamed Kibao,Mariam Ali Mohamed ameiomba serikali kufanya uchunguzi wa kifo cha baba yao huku akiomba familia iwe inapatiwa taarifa za uchunguzi huo na isipite muda mrefu bila matokeo ya uchunguzi kutoka huku akiomba majibu ya uchunguzi yawafikie familia kwa njia rasmi na sio kusikia kupitia vyombo vya Habari.
‘Tumesikia Mheshimiwa Rais,Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi wa kifo cha baba yetu,sisi kama familia tutakua tunapataje taarifa za uchunguzi huo najua kuna muda inakua ni vigumu kuwafikia viongozi wa juu huko serikalini hasa kwa kesi kama hii ni jambo nzito,tunachoomba ni ushirikiano wenu kama serikali kwetu sisi maana hata sisi hatujui nani amefanya huo utekaji na mauaji ya baba yetu.Muhimu tunaomba huo uchunguzi ufanyike kwa haraka ili ukweli ujulikane na haki ipate kutendeka.’ Alisema Mariam
Akizungumza na familia ya marehemu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni aliwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo ameiomba familia hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wamempoteza mpendwa wao huku akiwaomba wawe na Subira ili vyombo husika vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kutekwa na kuuawa kwa mzazi wao.
‘Mheshimiwa Rais amesikitishwa na kusononeshwa sana na tukio hili pamoja na serikali nzima tumesikitika sana ni jambo ambalo halikupaswa kutokea hasa katika nchi ambayo imekua inatajwa kuwa na amani,maelekezo ya Rais yashaanza kutekelezwa ili kubaini chanzo cha tukio hili,serikali yenu iko pamoja na nyie nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria kwahiyo kila mtu ana haki ya kuishi niwaombe sana muwe na mola wa Subira tumuombe Mwenyezi Mungu aijalie safari ya marehemu wetu iwe nyepesi na sisi tumuombe mungu mwisho mwema’ alisema Masauni
Waziri Masauni aliongozana na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga,Abdulrahman Shiloow na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mjini,Japhari Kubecha.Marehemu Ali Mohamed Kibao ameacha wajane wawili na watoto kumi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(wakwanza kulia) akitoa pole kwa Amina Muawiya ambae ni mjane wa aliyekuwa Kiongozi wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Marehemu Ali Mohamed Kibao baada ya kuitembelea na kuwafariji wakati wa msiba ambapo maziko yalifanyika jijini Tanga.