Ni kupitia Kiwanda cha East Africa Conveyor Supplies Limited
*Kiwanda kinauza vipuri hadi nje ya nchi
*Kutumika migodini, viwanda vya saruji na viwanja vya ndege
*Ni sehemu ya mpango wa ufungaji wa Mgodi wa Buzwagi
📍 Kahama.
Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya uzalishaji wa vipuri vya migodini na viwandani, baada ya Kiwanda cha kisasa cha East Africa Conveyor Supplies Limited (EACS) kilichopo Kahama, Shinyanga kuanza rasmi uzalishaji wa vipuri vya mitambo vinavyotumika kwenye migodi na viwanda mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya jitihada za Serikali katika kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji hapa nchini pamoja na Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini.
Akizungumza Mjini Kahama, Mkoani Shinyanga na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini, Mkurugenzi Mtendaji wa EACS, Peter Kumalilwa, alisema kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 Mtanzania na asilimia 50 Wageni kimeanza uzalishaji mwezi Mei 2023, ambako hivisasa vipuri vinavyozalishwa ni pamoja na steel conveyor frames, drop brackets, steel conveyor rollers, impact conveyor rollers, plastic na steel caps for conveyor rollers na bidhaa hizo zinauzwa kwenye migodi mbalimbali nchini Tanzania kama Barrick North Mara, Barrick Bulyanhulu na Buckreef, pamoja na migodi iliyo katika nchi jirani kama Kibali Gold Mine uliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Lumwana Mine uliopo nchini Zambia.
Kiwanda hicho kimejengwa katika eneo la Mgodi wa Buzwagi, ambalo hivi sasa lipo katika hatua za ufungwaji na kubadilishwa kuwa Eneo Maalumu la Uwekezaji Kiuchumi (Buzwagi Special Economic Zone) baada ya kukamilika kwa shughuli za uchimbaji madini zilizokuwa zikifanywa na Kampuni ya Barrick, ambapo uzalishaji huo wa vipuri unafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hali inayowezesha bidhaa zake kukidhi viwango vya ubora na ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa.
Kumalilwa alibainisha kuwa, malighafi nyingi zinazotumika katika kiwanda hicho, ikiwemo chuma na nondo, zinatoka katika viwanda vya ndani ya Tanzania, hivyo kuchangia katika ukuaji wa sekta ya viwanda nchini, sambamba na kupunguza gharama za uagizaji wa vipuri hivyo kutoka nje ya nchi kwa baadhi ya migodi hapa nchini.
Akifafanua kuhusu soko la bidhaa hizo, Kumalilwa alisema kwamba ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho umevutia masoko mengi, na wanatarajia kupanua biashara zao hadi nchi za Afrika Magharibi katika siku za usoni, na kwamba bdhaa hizo zinatumika katika viwanda vya saruji na viwanja vya ndege, huku akitoa rai kwa taasisi za kifedha kuwaunga mkono Watanzania ambao wamejikita kwenye uzalishaji wa vipuri au wanapanga kuanzisha viwanda kama EACS kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu na kuongeza kwamba, mikopo hiyo itawezesha Watanzania kushindana na wawekezaji wa nje ambao mara nyingi wana mitaji mikubwa.
Katika jitihada za kuendeleza sekta ya madini, Kumalilwa aliwasisitiza Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika migodi, badala ya kubaki mijini. “Nataka niwasisitize Watanzania kuwa madini ni maisha. Changamkieni hizi fursa. Tuje huku migodini tuangalie fursa gani tunaweza kufanya, hasa kwa kushirikiana na wawekezaji wa nje au kwa asilimia 100 ya Watanzania,” alisema Kumalilwa, akiongeza kuwa sekta ya madini inaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira na kuongeza viwanda nchini.
Kumalilwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Mining Industry Suppliers Association (TAMISA), alifafanua kuwa kuna shilingi trilioni 3.1 zinazozunguka kila mwaka katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, na iwapo wazawa hawatashiriki kikamilifu, fedha hizo zitaishia kwenda nje ya nchi. Aliwahimiza Watanzania kushikana mikono na kuanzisha viwanda vingi zaidi ili kusambaza bidhaa zinazohitajika katika sekta hiyo.
Aidha, aliishukuru Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yamewezesha kuzalisha bidhaa zinazokubalika katika soko la kimataifa. Alimshukuru pia Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, kwa kuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha kiwanda kinasimama.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Kahama Winnifrida Mrema alisema kuwa uwepo wa Kiwanda hicho ni jambo la kujivunia kwani ni moja kati ya miradi itakayosaidia kuliendeleza eneo la mgodi wa Buzwagi ambao upo kwenye hatua ya kufungwa baada ya shughuli ya uzalishaji wa dhahabu kukoma, hivyo kurahisisha upatikanaji wa vipuri ambavyo awali vilikuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi
Aliongeza kuwa, kupitia uwepo wa kiwanda hicho, watanzania watapata fursa ya kujifunza ujuzi kuhusu teknolojia mpya na kubainisha kuwa hatua hiyo ni moja ya uwekezaji mkubwa nchini unaoleta fursa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.
“Kuanzishwa kwa kiwanda cha EACS kinawakilisha hatua muhimu katika kuongeza thamani ya sekta ya madini na viwanda nchini Tanzania na kufungua milango kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji, katika Eneo Maalumu la Uwekezaji Kiuchumi” alisisitiza Mrema.
Naye, Meneja wa Ufungaji Mgodi wa Buzwagi Zonnastraal Mumbi alieleza kuwa katika mipango ya ufungaji mgodi huo, moja kati ya hatua za uendelezaji wa eneo hilo ni kuanzishwa kwa Eneo Maalumu la Uwekezaji Kiuchumi (SEZ) ambapo viwanda tofauti vitajengwa katika eneo hilo kwa matumizi bora ya ardhi na kulinda ajira kwa manufaa ya mnyororo mzima wa shughuli za kiuchumi katika mji wa Kahama huku akiwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo.