Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimeunda Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini (MELL) ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia na kufuatilia tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika chuo hiki.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mratibu Msaidizi wa Kitaifa wa Mradi wa HEET, Dkt. Evaristo Mtitu, amesema kamati hii inatakiwa kuandaa ripoti zote zinazohusiana na utekelezaji wa Mradi wa HEET na ripoti hizo ndizo zitakazo kaguliwa na mamlaka mbalimbali zilizoidhinishwa kufanya hivyo pamoja na wafadhili wa mradi ambao ni Benki ya Dunia.
“Huu ni mradi wa kimkakati hivyo malengo mliyojiwekea ambayo yalikubaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Dunia mnatakiwa kuyaangalia yatimizwe kwa uadilifu, Kamati ya MELL ni jicho la utekelezaji wa huu mradi, hii ni dhamana kubwa sana mliyopewa,” amehimiza Dkt. Mtitu.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda, amesema kamati ya ufuatiliaji na tathmini ni muhimu sana wakati huu ambao chuo kinafanya utekelezaji wa Mradi wa HEET hasa kipindi hiki ambacho ujenzi wa majengo ya maabara unaanza kwenye kanda saba.
“Huu mradi ni wetu, tumekuwa tukipata changamoto na gharama kubwa tunapofika kwenye swala la matumizi ya maabara, Mradi wa HEET unakwenda kutatua tatizo hilo hivyo kamati hii ikasimame vyema na imara kuhakikisha hakuna kinachoharibika kwa namna yoyote ile kwa kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kufuata matakwa ya mradi,” amesema Prof. Bisanda.
Akiongea katika uzinduzi huo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Tafiti na Huduma za Kitaalam na Mratibu wa Mradi wa HEET chuoni, Prof. Alex Makulilo, amesema baada ya uzinduzi wa kamati hii, itahakikisha usimamizi na ufuatiliaji wa mradi kuimarika na chuo kinafuata vyema matakwa ya mradi, Wizara na Benki ya Dunia ili mradi ufikie mafanikio kama inavyotarajiwa.
Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini (MELL) ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, imeundwa ikiwa na wajumbe saba kutoka ndani ya chuo hiki ikiongozwa na Mwenyekiti Ndg. Benjamin Bussu, akifuatiwa Makamu Mwenyekiti Dkt. Emmanuel Mallya na Katibu ambaye ni Dkt. Juliana Kamaghe. Kamati itakuwa na jukumu mama la kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa mradi wa miaka mitano wa HEET unaotekelezwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia udhamini wa Benki ya Dunia unaolenga kuimarisha taasisi za elimu ya juu katika maeneo ya miundombinu, ufundishaji na ujifunzaji ambapo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimepata takribani Dola Milioni 9 Kimarekani.
Kamati hii imezinduliwa rasmi na Dkt. Evaristo Mtitu, makao makuu ya Chuo Kinondoni jijini Dar es Salaam, Septemba 12, 2024, ikiwa ni takwa la mradi lakini pia ina jukumu la kusimamia na kufuatilia mradi katika ngazi ya taasisi na kuandaa ripoti ya utekelezaji wa mradi huo.
Social Plugin