Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA WAPEWA ELIMU KUHUSU UGONJWA WA KIHARUSI 'STROKE'



Na George Mganga, SHINYANGA RRH

KUTOKANA na ongezeko la watu wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa miaka ya hivi karibuni, elimu ya Afya kuhusiana na Ugonjwa wa Kiharusi (Stroke), imetolewa leo Septemba 11, 2024 kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.


Akitoa elimu hiyo, Daktari Bingwa Bingwa wa Magonjwa ya ndani na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Luzila John, ameeleza lengo mama la elimu hiyo ni kuwasaidia watumishi ili waweze kulinda afya zao.

Dkt. Luzima amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza si ya wananchi wa kawaida pekee, bali ni kwa kila rika na kila mtu, akibainisha kuwa watumishi wana haki ya kukumbushwa ili kulinda afya zao pamoja na kuwasaidia wagonjwa wanaokuja hospitalini.

“Nimetoa elimu hii kwa ajili ya kunusuru afya za watumishi ili waweze kutambua madhara ya Kiharusi.

“Elimu hii si kwa wananchi walio nje ya Hospitali pekee, hata watumishi wenyewe wanapaswa kuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kufahamu maendeleo yao”, amesema.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Luzila amebainisha kuwa watu milioni 15 hupata Kiharusi kila mwaka, akieleza katika idadi hiyo, asilimia 30 hufariki, 30 hupona wakiwa na kilema, zilizobaki hupona na kurudi kwenye hali yao ya kawaida.

Kwa upande wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Luzila amebainisha Hospitali hulaza wagonjwa 20 kwa kila mwezi, huku akisema kwa takwimu za miezi mitano (Februari hadi Juni) mwaka huu, hospitali ilipata jumla ya wagonjwa 108 baada ya kufanyiwa vipimo vya CT SCAN.

Aidha, Luzila ameyataja magonjwa ya Shinikizo la Juu la Damu, Kisukari na Magonjwa ya Moyo, kuwa ndiyo magonjwa sababishi ya Kiharusi, hii ikichagizwa na mtindo wa maisha ambao watu wanaishi nao kwa sasa.

Vilevile, Luzila ameshauri watu wawe na desturi ya kufika kwenye vituo vya afya mara kwa mara kwa ajili ya kupata vipimo, pamoja na kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuulinda mwili na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kwa upande mwingine, Luzila ameshauri watu kuacha matumizi holela ya pombe, uvutaji wa sigara na tumbaku sababu ndiyo visababishi vikubwa vinavyopelekea mtu kupata magonjwa hayo ikiwemo kiharusi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com