Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIKOA, HALMASHAURI ZAAGIZWA KUSHIRIKI MAONESHO YA VIWANDA


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza mikoa na hamlashauri zote nchini kuhakikisha viwanda vilivyo katika mamlaka zao vinashiriki katika maonesho ya biashara ya kimataifa.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 26, 2024 Jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango katika ufunguzi wa Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania mwaka 2024.

“ Naagiza Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha Viwanda vilivyo katika Mamlaka zao vinashiriki kuonesha bidhaa wanazozalisha ili bidhaa hizo ziweze kutafutiwa masoko ya ndani na nje ya nchi yakiwemo ya ukanda wa EAC na SADC kwa lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji hususani katika sekta ya viwanda ili kukuza uchumi wa Viwanda na nchi kwa ujumla.

“ Tutakumbuka kuwa andiko letu la Blueprint ambalo limeainisha changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuondoa changamoto hizo. Kazi hiyo ilianza katika Awamu ya Tano na nipende kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuhakikisha kuwa changamoto zinazoikabili biashara na uwekezaji ikiwemo katika sekta ya viwanda zinaendelea kutatuliwa.” Amebainisha Dkt. Biteko.

Aidha, amewahamasisha wafanyabishara na wenye viwanda nchini, kuendelea kushirikiana na Serikali na Taaasisi zake, katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda nchini tunazitatua kwa pamoja ili kukuza uchumi wa nchi.

Pia, Dkt. Biteko amebainisha kuwa maonesho hayo yatakuwa na tija zaidi ikiwa wahusika wataaelezana ukweli ili kuwa namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya viwanda na biashara nchini. Sambamba na kuzitaka taasisi zote zinazosimamia ubora wa bidhaa kuhakikisha zinashiriki katika maonesho hayo ili kutoa elimu kwa umma na kutatua changamoto zinazoikabili katika sekta hiyo.

“ Nitumie fursa hii kuzielekeza taasisi zote za Serikali za udhibiti na wezeshi katika sekta ya biashara, viwanda na uwekezaji kama BRELA, TBS, TMDA, TIC, WMA, FCC, OSHA, SIDO nakadhalika, kuhakikisha zinashiriki katika Maonesho haya ili kuendelea kutoa elimu kwa umma na kutumia fursa hiyo kutatua changamoto zinazokabili sekta ya viwanda na wafanyabiashara kwa ujumla nchini.”Amesema Dkt. Biteko.
Akizungumzia bidhaa zinazoingizwa kwa magendo nchini kupitia Mkoa wa Dar es salam, Dkt. Biteko ameitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es salaam kudhibiti njia za magendo huku akiwataka wafanyabiashara kuona fahari kulipia kodi bidhaa zinazoingizwa nchini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa awali Tanzania ilikuwa na uhaba wa umeme na kuwa kwa sasa nchi inajitosheleza katika nishati ya umeme.

“ Sasa tuna ziada ya umeme ya kutosha hata mkienda kuangalia leo matumizi ya umeme tunaozalisha kwa kutumia gesi yamepungua kwa sababu tuna umeme wa kuzalisha wa maji wa kutosha kwa hiyo hatuna tatizo la umeme kwa kuwa Serikali imeweka mifumo mizuri, tumieni umeme huu kwa ajili ya kusalisha bidhaa.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wenye viwanda nchini kutumia fursa ya Maonesho hayo kushiriki kwa wingi ili kujifunza teknolojia mpya za kisasa, kutangaza bidhaa zao na kuufahamisha umma na walaji juu ya ubora na faida za kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda mchini. Aidha, Serikali inatambua kwamba sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda huku yenyewe ikiwekeza katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.

Pia, Dkt. Biteko amewahamasisha wadau wa sekta ya viwanda kuendelea kutoa michango yao ya mawazo ya namna ya kuboresha Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo. Pamoja na kuwataka Watanzania kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wazalendo katika ngazi za mitaa na vijiji.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe amesema kuwa maonesho hayo yamehusisha washiriki 250 kutoka kampuni za ndani na nje ya nchi na kutaja lengo la maonesho hayo kuwa ni kujifunza na kubadilishana mawazo katika sekta ya viwanda.

“ Tunategemea mwakani kuona hamasa zaidi kwa wazalishaji wadogo ambao ni zaidi ya asilimia 90, naomba niwahakikishie Wizara ya Viwanda itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wanaounga mkono sekta ya viwanda nchini.” Amesema Mhe. Kigahe.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa maonesho hayo yahimize uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi zenye ubora ili zishindane na masoko ya nje.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade, Prof. Ulingeta Mbamba amesema kuwa maonesho hayo ya pili yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Tanrtrade na kuwa ni muhimu kwa vile yanahamasisha wazalishaji wa bidhaa za viwanda na wazalishaji binafsi kwa ajili ya kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mwenyekti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Bw. Paul Makanza amesema kuwa kuna fursa ya kutengeneza bidhaa na kuuza nje ya nchi na kuwa maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kujenga mtandao wa wateja na wafanya biashara na kujifunza kutoka kwa wageni.

Awali Dkt. Biteko ametembelea mabanda mbalimbali na kuona magari yanayotumia umeme yanayozalishwa nchini na Kampuni ya KAYPEE Motors Limited pamoja na ndege zinazotengenezwa mkoani Morogoro na kmpuni kutoka nchini Czech.

Maonesho haya ya Pili (2) ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania 2024 yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 01, 2024.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com