MKUTANO WA OACPS KUSAIDIA KUWEKA MIKAKATI MADHUBUTI YA KUINUA SEKTA YA UVUVI TANZANIA


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kufanyika kwa mkutano wa OACPS nchini Tanzania kutasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuinua sekta ya uvuvi na kuchechemua uchumi wa taifa kwa ujumla.

Waziri Ulega amebainisha hayo wakati akifungua Mkutano wa Wataalam wa Uvuvi wa Bahari na Maji baridi kutoka Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) jijini Dar es Salaam Septemba leo 9, 2024.

“Lengo la mkutano wa OACPS ni kujadili mambo mbalimbali yanayohusu ustawi wa bahari na maji baridi na kuweka mikakati ya kunusuru hatma ya uvuvi na wavuvi wenyewe”, amesema

Kwa mujibu wa Waziri Ulega, mkutano huo wa OACPS utakuwa na faida nyingi hapa nchini ikiwemo Mashirika yaliyoshiriki mkutano huo kuangalia namna ya kuwawezesha wavuvi wadogo kuboresha shughuli zao kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi.

Kuwawezesha wavuvi kutumia teknolojia za kisasa za uvuvi ili kuwaondoa wavuvi hao kutoka katika uvuvi wa kienyeji na wapate vifaa vya kisasa vya uvuvi.

Aliongeza kwa kusema kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa wadau wa uvuvi kubadilishana uzoefu ili kwa pamoja waweze kuboresha shughuli zao.

“Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya jitihada kubwa katika kujaribu kutatua changamoto zinazowakumba wavuvi wadogo na wakuzaji viumbe maji ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya uvuvi, kuboresha teknolojia, kutoa vifaa vya kisasa kwa ajili ya shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kupata mitaji na masoko”,

Aidha, Waziri Ulega alibainisha kuwa Tanzania itaendelea kusimamia ipasavyo juhudi zitakazohakikisha usimamizi endelevu wa raslimali za bahari na maji ya ndani zinazofanyika kupitia mikakati mbalimbali iliyoandaliwa ikiwemo kupitia Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi, Sera ya Uchumi wa Buluu, na juhudi zetu zinazoendelea za kupambana na uvuvi Haramu na usioripotiwa (IUU), ambayo inalenga kuhakikisha kuwa rasilimali za maji hasa bahari, maziwa na mito zinaendelea kuwa endelevu na kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post