Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, ametoa maagizo maalum kwa viongozi wa chama hicho, akiwahimiza kuhakikisha kuwa wanachama wanandikishwa kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.
Mongella alitoa maagizo hayo alipomtembelea Balozi wa Shina namba 3, Safina Masanja Kitundu, katika tawi la Buduhe, Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Amesisitiza kuwa CCM ni chama chenye heshima na nafasi muhimu katika kulinda mustakabali wa nchi. Kwa hivyo, alihimiza kuhakikisha kuwa uandikishaji wa wanachama unafanywa kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa kuandikisha wanachama wengi katika jumuiya za UWT, Wazazi, na Vijana, ili kukifanya chama kiwe imara.
Mongella pia alibainisha kuwa siri ya mafanikio ya chama ni kujikita kwenye mashina na kufanya kazi kwa karibu na mabalozi. Ziara yake ya siku saba mkoani Shinyanga inatarajiwa kuhitimishwa baada ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2024 na kuimarisha uhai wa chama.
Social Plugin