MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameshiriki mahafali ya kwanza ya kihistoria ya shule mpya ya msingi Mtaturu iliyopo kijiji cha Ikungi huku akiwatakia kheri wanafunzi wa darasa la saba walioanza mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi hii leo na kuahidi motisha kwa mwanafunzi atakayepata Alama A.
Katika salamu zake alizozitoa shuleni hapo Mtaturu amesema mwanafunzi atakayepata alama A atapewa madaftari makubwa 10,viatu pea moja na soksi pea tano.
Aidha,amechangia kompyuta moja na printa ili kurahisisha maandalizi ya masomo kwa walimu shuleni na jezi mbili kwa ajili ya michezo kwak uwa michezo na elimu ni mapacha.
“Nawapongeza wananchi na wazazi kwa kusimamia miradi ikiwemo kufyeka pori na kung'oa visiki,kusogeza mchanga na mawe iliyorahisisha kutekeleza mradi huu wa shule mpya baada ya kupokea Kiasi cha zaidi ya Shilingi 500,”.amesema.
Mtaturu amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwak upeleka fedha nyingi za miradi walizozipokea kwenye jimbo la Singida Mashariki kwenye sekta ya elimu,afya,miundombinu ya umeme,maji na barabara na kuahidi kuendelea kumuunga mkono wakati wote.
Akisoma risala Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Kitila Mkumbo amemshukuru Mbunge Mtaturu kwa kuwasemea changamoto zao serikalini na hatimae wamepokea mradi mkubwa wa madarasa 16,Jengo la utawala na Matundu ya Vyoo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 500.
Ameeleza changamoto walizonazo ikiwemo vifaa vya Tehama,Kompyuta na mashine ya kunakilisha kwa ajili ya kurahisisha maandalizi ya masomo shuleni.
Akitoa Salamu za wananchi Mwenyekiti wa Kijiji Athumani Kitui amemshukuru sana mbunge kwa jitihada zake za kupaza sauti Bungeni na hatimae leo Ikungi imebadilika kwa kuwa kila eneo ni miradi kila sekta.
“Tunasema unatufaa,tutaendeleaa kukutuma ili tufaidike zaidi,tunakuomba utupelekee salaam zetu kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba Ikungi tunaridhika na uongozi wake,”.amesema.