WATAFITI WATAKIWA KUTAFSIRI KWA LUGHA RAHISI MATOKEO YA TAFITI ZAO KUHUSU MTO MARA

 
Na Mwandishi Wetu-  Narok Kenya
Wanasayansi na watafiti wanaofanya tafiti kuhusu faida za uhifadhi wa bonde la mto Mara wametakiwa kutafsiri kwa lugha rahisi matokeo ya tafiti zao ili ziweze kueleweka  kwa jamii husika hatua ambayo itakuwa na mchango chanya kwenye uhifadhi wa bonde hilo.

Akizungumza kwenye kongamano la pili la  wanasayansi leo Septemba 14,2024 katika Kaunti ya Narok nchini Kenya kujadili utunzaji wa bonde la mto Mara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Mara,Profesa Patrick Lumumba kutoka chuo Kikuu cha Nairobi amesema matokeo ya tafiti nyingi yameandikwa kwa lugha ngumu ambazo hazieleweki hasa kwa jamii zinazozunguka bonde la mto huo.

Amesema Bonde la Mto Mara linakabiliwa na changamoto kubwa za uharibifu wa mzingira pamoja na mabadiliko ya tabia nchi na kwamba ili changamoto hizo ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu suala la ushiriki wa  jamii ni la muhimu.

"Ni lazima tuwe na maneno ya kueleweka,tuwe na misamiati inayotamkwa na kueleweka katika mitaa na vijiji vinavyozunguka bonde,tutafsiri  manneo magumu hata kwa kilugha cha jamii husika ili yaeleweke  kuna maneno mengi mfano neno baianua, ikolojia, na mengine mengi," amesema .

Amesema wananchi wakielewa kwa kina madhara na nini cha kufanya kwaajili ya ulinzi wa bonde hilo upo uwezekano mkubwa wa wao kushiriki kwa  kiwango kikubwa katika ulinzi wa bonde hilo hivyo kuwa  na matokeo chanya.

Profesa Lumumba amesema  mamlaka husika pia zinatakiwa kujihoji kama zinafanya wajibu wao kikamilifu katika ulinzi wa bonde hilo kufuatia uwepo wa shughuli za kibinadamu zinazotishia  uhai wa bonde la mto Mara. 

"Tujihoji kabla ya kutoa vibali vya uwepo wa viwanda na hata kufanya utafiti kujiridhisha juu ya viatilifu vinavyotumika kwenye kilimo kando ya bonde hilo kama vitu hivyo ni rafiki  kwa uhai wa bonde na hili linapaswa kufanywa kwa pamoja  baina ya nchi zetu mbili yaani Kenya na Tanzania na Afrika Msahariki jwa ujumla," ameongeza 


Mkuu wa mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema jukumu la ulinzi wa rasilimali hiyo ni la kila mdau hivyo suala utekelezaji  wa makubaliano ya midahalo ya wanasayansi ambayo imeanza kufanyika mwaka jana inatakiwa kusimamiwa na kutekelezwa kwa pamoja.

"Kesho ya bonde la mto Mara iko kwenye mikono yetu,na hili linawezekana tukiamua kwani tuna wajibu wa pamoja wa kulinda ustawi na uendelevu wa bonde hili kwa manufaa ya watu wetu kutoka nchi zote mbili," amesema Mtambi

Mtambi amesema madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu ni katoka bonde hilo makubwa lakini  yanaweza kuepukika endapo ushauri wa tafiti za kisasanysi zilizowasilishwa  utafanyiwa kazi kwa pamoja na kwa wakati.


Amesema serikali mkoani Mara itahahkilisha inashirikiana na wanachi na wadau wengine katika ulinzi  bonde hilo kwa maelezo kuwa uharibifu wa mazingira kwa ujumla ni  sawa na hukumu ya kifo kwa kizazi kijacho.


Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la ziwa Victoria,  Dk Masinde Bwire amesema ustawi wa  bonde la mto Mara  una mchango wa moja kwa moja kwa uchumi wa watu na uendelevu wa sekta ya utalii kwa nchi zote  zote mbili.

Amesema changamoto zinazokabili bonde hilo zinapaswa kujadiliwa kwa pamoja kwa kushirikisha watafiti, watunga sera pamoja watejelezaji na wadau wote kushiriki ili kuja na makubaliano ya pamoja juu ya namna ya ulinzi wa bonde hilo.

"Bonde la mto Mara sio rasilimali muhimu kwa ikolojia pekee bali  pia ni nguzo muhimu ya kiuchumi kwa mamilioni ya watu wa nchi zetu wanaolitegemea kama rasilimali muhimu katika maisha yao hivyo ulinzi wake ni jambo la lazima," amesema Dk Bwire


Akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Brian Ndungu kutoka Chuo Kikuu cha Maasai Mara amesema bonde la mto Mara linakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwepo kwa mikakati ya kutosha ya utunzaji wa mazingira ya bonde  pamoja na ushiriki hafifu wa wadau.

Amesema changamoto hizo zinahusu  uharibifu wa uoto wa asili katika bonde hilo unaofanywa kwa upande wa Tanzania na Kenya pamoja na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi mambo ambayo yanahitaji ushiriki wa pamoja kutoka kwa wadau wote.
   



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post