Na Dotto Kwilasa, DODOMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano Maalum wa Mazingira kuainisha namna bora ya kufikia matokeo tarajiwa kwa kutafuta majibu ya changamoto za kimazingira zilizopo nchini hususani katika changamoto ya uimarishaji wa mfumo wa usimamizi wa mazingira.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano Maalum wa Viongozi, Wataalamu na Wadau wa Mazingira kuhusu Mwelekeo wa Mazingira Nchini unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Amesema mafanikio yamepatikana katika kuweka sera na kanuni, isipokuwa kuna mapungufu ya kisheria kuhusu nguvu na wigo wa Baraza la Taifa la Usimamizi Mazingira (NEMC) hali ambayo inapelekea licha ya maelekezo yanayotolewa na viongozi kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa mazingira nchini lakini utekelezaji umekuwa hafifu katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri na vijiji.
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa utoaji elimu ya Biashara ya kaboni ambayo ni fursa katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Amesema elimu inapaswa kutolewa kuhusu mikataba bora ya hewa ya kaboni iweje kwa maana ya mapato na teknolojia kutoka nchi zilizoendelea ambao ndiyo wazalishaji wakubwa wa hewa ya kaboni.
Aidha kufahamu wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kwa nchi kama Tanzania ambazo zina Masinki makubwa ya Kaboni ikiwa ni pamoja na eneo kubwa la bahari na maziwa, ardhi oevu na eneo kubwa la hifadhi lililotengwa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema katika dhana ya uchumi wa buluu bado utafiti wa kutosha unahitajika unaolenga kubaini rasilimali nyingi zinazopatikana katika maji na menejimenti yake ikiwemo rgesi asili, madini, viumbe hai, matumbawe n.k.
Makamu wa Rais amesema Taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali za mazingira ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na tabiawatu ikiwemo ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa misitu, kilimo kisicho endelevu na ufugaji holela usiozingatia uwiano wa idadi ya mifugo na maeneo ya malisho.
Ametaja mambo mengine yanayochangia uharibifu wa mazingira ni pamoja na utupaji taka hovyo, uharibifu wa vyanzo vya maji, uvamizi wa ardhi oevu pamoja na matumizi ya Nishati chafu.
Ameongeza kwamba yapo mambo mbalimbali yanayochangia hali mbaya ya mazingira nchini ikiwemo Sheria kinzani kama vile mkaa kuwa chanzo cha mapato cha Wakala wa Misitu (TFS) hii inahamasisha utoaji wa vibali vya kukata miti. Pia vitalu vichache vya miti, miti inayopandwa kutotunzwa, kutotosheleza kwa miundombinu ya ukusanyaji na uhifadhi wa taka, uchache wa viwanda vya kurejereza taka pamoja na gharama za teknolojia ya kijani.
Makamu wa Rais amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuandaa Sera, Kanuni, Mikakati, programu za upandaji miti, kampeni za usafi na hasa mijini na kwenye fukwe, kuhamasisha utunzaji wa mazingira kupitia vyombo vya habari, mashindano ya mikoa na halmashauri katika usafi, ushiriki katika siku ya mazingira duniani na programu ya jenga kesho iliyo bora (BBT).
Mkutano Maalum wa Mazingira unafanyika kwa siku mbili tarehe 09 – 10 Septemba 2024 ukiwakutanisha Viongozi, Wataalamu, Wadau wa Mazingira pamoja na wananchi mbalimbali kwa lengo la kujadili mwenendo wa hali ya mazingira nchini na kukubaliana hatua za kuchukua ili kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile Mkutano huo unalenga kuzikumbusha Wizara za Kisekta, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta ya Umma, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia wajibu wao wa kusimamia, kuhifadhi na kutumia fursa zilizopo katika mazingira.