Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Nigeria na Arsenal ya England, Nwankwo Kanu ametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila kwa lengo la kuwajulia hali na kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo na kuangalia maeneo wanayoweza kushirikiana.
Kanu ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kanu Heart Foundation ametembelea kitengo cha uchunguzi wa magonjwa ya moyo, wodi ya kulaza wagonjwa ya moyo pamoja na kutembelea wodi ya watoto wanaopatiwa joto na mama zao kufuatia kuzaliwa wakiwa na uzito mdogo maarufu kangaroo.
Kanu amebainisha kuwa taasisi yake imeshatoa ufadhili wa matibabu ya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 90 ambao walisafirishwa kwenda India ambapo pia amewapongeza watoa huduma wa afya kwa kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa watu wanahudumiwa na kurejea katika hali zao za awali.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji MNH, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Godlove Mfuko amesema Muhimbili Mloganzila inahudumia takribani wagonjwa 1000 kwa siku, kati ya hao wenye changamoto za moyo ni takribani 60.
Dkt. Mfuko ameongeza kuwa kupitia mpango wa Samia Scholarship hospitali hiyo imeendelea kunufaika kwa kuendelea kutatua changamoto za upungufu wa watumishi hususani katika eneo la magonjwa ya moyo na kuendelea kuimarisha huduma za magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo.
Kanu amekuja nchini kwa uratibu wa Vodacom Foundation ambao kwa pamoja mwaka huu wanafadhili mashindano ya kuendesha baiskeli ‘twende Butiama’ yenye lengo la kukusanya fedha kusaidia jamii, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere ambaye alipambana na ujinga, maradhi na umasikini.
Social Plugin