Na Mwandishi Wetu
Wajasiriamali wadogo wapatao 500 wanaojihusisha na uchimbaji na uchakataji kokoto Jijini Dar es Salaam wamewezeshwa vifaa kinga na kupatiwa mafunzo ya usalama na afya ili kujiepusha na ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi vilivyopo katika mazingira ya kazi.
Uwezeshaji huo umefanywa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ikiwa ni utekelezaji wa jukumu lake la msingi la kujenga uelewa wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.
Makundi yaliyonufaika na uwezeshaji huo kwa hatua ya awali ni wale ambao wanafanya shughuli zao katika maeneo ya Boko Magereza, Kata ya Bunju katika Wilaya ya Kinondoni na maeneo ya Mjimwema katika Wilaya ya Kigamboni.
Akifungua program hiyo ya uwezeshaji wa wachimbaji wadogo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema pamoja na changamoto zinazowakumba wachimbaji na wachakataji wadogo wa kokoto ikiwemo matumizi ya teknolojia duni na ukosefu wa mitaji, mchango wa wachimbaji hao katika uzalishaji wa malighafi za ujenzi ni mkubwa.
“Ninapenda kuwatia moyo kwamba changamoto zilizopo katika sekta hii hazitakuwa za kudumu. Hivyo, niwaombe tushirikiane kuchukua hatua za kuleta mabadiliko chanya katika sekta hii ikiwemo kuhakikisha kwamba shughuli zote zinafanyika katika mazingira salama na tija inaongezeka kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa,” ameeleza Waziri Kikwete na kuongeza:
“Kwa upande wetu kama serikali tumeshaanza kuchukua hatua kwa kuanzia na kuwapa elimu kama inavyofanyika leo lakini tutaendelea na hatua nyingine ikiwemo kutengeneza mazingira wezeshi yatakayopelekea tija kuongezeka ikiwemo kuhakikisha mnapata mitaji kwa ajili ya kununua zana za kisasa ikiwa ni pamoja na kuanzisha shughuli mbadala.”
Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya Masuala ya Kazi, Bi. Mary Ngelela Maganga, aliyehudhuria baadhi ya madarasa ya semina iliyokuwa ikiendeshwa na wataalam wa OSHA, amesema kwa kuzingatia mchango wa wajasiriamali wadogo katika maendeleo ya nchi, Taasisi yake ya OSHA imeona ni muhimu kuwapa elimu ya usalama na afya wachimbaji hao ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema mafunzo yanayotolewa na wataalam wake kwa wachimbaji wadogo yamejikita katika kuwawezesha kutambua vihatarishi vinavyoambatana na shughuli zao ikiwemo vumbi, joto kali na mtindo wa ufanyaji kazi usiozingatia taratibu za igonomia.
Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA ameeleza kuwa mafunzo hayo yanaambatana na utoaji wa vifaa kinga muhimu vilivyogharamiwa na serikali ili kuwahamasisha wachimbaji hao kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa kinga katika kazi zao.
Vifaa kinga vilivyotolewa kwa wajasiriamali hao ni pamoja na barakoa, vikinga mikono (gloves), vizibao vinavyoakisi mwanga (reflective vests) kutambulisha uwepo wa mfanyakazi mahali pa kazi pamoja na masunduku ya huduma ya kwanza.
Wajasiriamali walionufaika na uwezeshaji huo akiwemo Bi.Berena Bilal, wameishukuru serikali kupitia OSHA kwa uwezeshaji waliopata.
“Kwa niaba wajasiriamali wenzangu naishukuru OSHA kwa kutuelimisha na kutuletea vifaa kwani awali tulikuwa hatufahamu hatari zinazotuzunguka lakini leo wataalam wametufahamisha na kutupatia mbinu za kudhibiti hatari hizo,” amesema Bi Berena Bilal.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani
Kikwete, akizungumza
na wachimbaji na wapondaji wa kokoto waliowezeshwa na OSHA kwa kupatiwa mafunzo
ya usalama na afya pamoja na vifaa vya kujikanga katika machimbo ya Masasi,
Mjimwema, Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Social Plugin