Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF. SHEMDOE ASHIRIKI UVUNAJI SAMAKI MRADI WA KISOKO

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kulia), akishiriki shughuli ya uvunaji Samaki wa Vizimba, iliyofanyika eneo la Mradi wa Kisoko, Septemba 25, 2024, Mwanza.

****************

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, ameshiriki shughuli za uvunaji wa samaki aina ya Sato katika Vizimba vilivyopo eneo la Kisoko ili kushuhudia hali ya Samaki hao ikiwemo ukubwa wake na shughuli za uuzaji wa Samaki hao ulivyofanyika katika eneo hilo.

Akizungumza, leo Septemba 25, 2024 mkoani Mwanza alipotembelea eneo hilo la Mradi wa Ukuzaji Samaki kwa njia ya Vizimba, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Shemdoe amesema samaki hawa walikuwa wadogo sana, ila leo hii wanavunwa wakiwa wakubwa kiasi cha kwamba wanafaa kuingia sokoni na kuliwa.

"Hii mbegu ya samaki ilikuwa ndogo sana na haishikiki, ila leo hii tunavuna ikiwa kitu ambacho tunakiona hapa kwa mara ya kwanza, na hii yote ni Shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha ili ziweze kutumiwa na Vijana hawa wa Jenga Kesho Iliyo Bora - BBT katika uzalishaji huu wa bidhaa za uvuvi" amesema Prof. Shemdoe

Aidha, Prof. Shemdoe alisema Tarehe 30 Januari mwaka huu Mhe. Rais alizindua Mradi huu ambao ulikuwa na vizimba 222 na Boti 160 ambazo zimekopeshwa katika maeneo ya ziwa Viktoria na Bahari ya Hindi, na kutokana na mkopo huo, leo hii kinaonekana kilichopatikana ambacho ni uwepo wa Samaki wengi na wakubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Imani Kapinga, amesema lengo la Mradi huu ilikuwa ni kufikisha gramu 300, ila ni habari njema kuwa kuna samaki wenye gramu 400 hadi 500, kiasi kwamba malengo yamevukwa.

Vilevile Dkt. Kapinga amesema, mvuno wa leo ni wa kikundi kimoja kati ya vikundi 12 vilivyopo hapa eneo la Kisoko, ila vikundi vingine vitaendelea kuvuna kuanzia mwezi wa kumi na moja hadi wa tatu mwakani.

Naye, Afisa Maendeleo ya Biashara Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TAD, Bw. Samson Siyengo amesema Mkoa wa Mwanza umenufaika kwa kiasi kikubwa kwani zaidi ya Bilioni 4 zimetolewa kwa Vijana wa Jenga Kesho Iliyo Bora waliopo Mwanza.

Mnufaika wa Vizimba ambaye pia ni Katibu wa Kikundi kilichovuna samaki leo, Kikundi cha Vijana Nguvu Kazi, Bw. Pius Mtenya ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassani kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Mheshimiwa Abdallah Ulega kwa kuwapa Mkopo husio na Riba ili waweze kufanya shughuli za ukuzaji viumbe maji ili waweze kujipatia kipato.

Vilevile, Bw. Mtenya Amesema katika uvunaji wa leo wanataraji kupata jumla ya tani 19.8, katika vizimba 6, ikimaanisha kila kizimba kitatoa tani 3.3, na hii inaonyesha ni jinsi gani watakavyopata faida kutokana na Mradi huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe (wa kwanza kushoto), akiwa ameshikiria Samaki aina ya Sato waliovunwa kwenye Vizimba, ni mara baada ya kushiriki shughuli za uvunaji Samaki hao, uliyofanyika eneo la Mradi wa Kisoko, Septemba 25, 2024, Mwanza
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kulia), akitazama mzani kwa umakini baada ya kununua samaki, mara baada ya kushiriki shughuli za uvunaji samaki hao, uliyofanyika eneo la Mradi wa Kisoko, Septemba 25, 2024, Mwanza
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kulia), akizungumza na wadau wa Ukuzaji viumbe maji na wakishiriki wa shughuli za uvunaji Samaki wa Vizimba, iliyofanyika eneo la Mradi wa Kisoko, Septemba 25, 2024, Mwanza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com