Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RABIA AELEZA MAFANIKIO YA CCM, SERIKALI KWA WANADIASPORA UINGEREZA


Tarehe 28 Septemba 2024, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndg. Rabia Abdalla Hamid, amekutana na Wanadiaspora na wanachama wa CCM nchini Uingereza.

Lengo la kukutana lilikuwa kuimarisha uhusiano baina ya Wanadiaspora, Chama Cha Mapinduzi na serikali, pia kuwapa taarifa kuhusiana na shughuli na kazi zinazoendelea kufanywa na serikali ya CCM katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana nchini.

Katika maelezo yake, Ndg. Rabia ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, aliwaeleza Wanadiaspora hao namna serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyoboresha huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu, umeme na maji.

Alitoa mfano wa maendeleo makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya kwa kujengwa hospitali na vituo vya afya bora vinavyotumia vifaa tiba vya tekinolojia ya kisasa.

Ndg. Rabia aliwaambia Watanzania hao wanaoishi Uingereza kwamba, jitihada hizo za serikali zimelenga kuboresha kiwango cha matibabu nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kusogeza matibabu ya kibingwa karibu na wananchi.

Alifafanua kwamba lengo ni kupunguza gharama za wananchi kusafiri umbali mrefu au nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ya kibingwa, hivyo kuokoa fedha ambazo watazitumia katika shughuli nyingine za kujiletea maendeleo.

Akizungumzia maendeleo ya kiuchumi, Ndg. Rabia alitoa mifano ya miradi ya kimkakati ya miundombinu ambayo imetekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na serikali ya CCM, chini ya uongozi makini na thabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alitaja baadhi ya miradi kuwa ni ujenzi wa barabara, reli ya kisasa maarufu SGR, viwanja vya ndege, na uboreshaji wa bandari ili kuziwezesha kutoa huduma kwa ufanisi na tija.

Alisema miundombinu bora itakuza na kuimarisha uchumi wa taifa kwa kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, hivyo kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi kikiwemo kilimo.

Alisema SGR na Mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ni muhimu kwa uchumi katika kuongeza uwezo wa usafirishaji bidhaa kwa haraka na gharama nafuu, pamoja na kupatikana kwa umeme wa uhakika ukaochochea ongezeko la viwanda nchini.

Aliwahakikishia Wanadiaspora hao kwamba CCM kinatambua umuhimu wao katika kuchangia maendeleo ya taifa, na kwamba ilani ya CCM imeweka wazi kutambua nafasi muhimu waliyonayo kwa maendeleo ya nchi.

Mkutano huo uliendeshwa kwa majadiliano ya wazi, ambapo Wanadiaspora waliuliza maswali na kutoa maoni kuhusu mambo yanayoendelea nchini.

Katibu wa NEC, Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndg. Rabia, aliwashukuru Wanadiaspora kwa mchango wao wa kiuchumi na kijamii kwa taifa, na kuwaomba waendelee kuunga mkono jitihada za serikali zinazohakikisha nchi inapata maendeleo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com