RAIS SAMIA : WAKATAENI WANAOFIKA KWENYE MAENEO YENU KUWASHAWISHI KUHARIBU AMANI NA UTULIVU



Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Watanzania hawapaswi kushawishika kwa namna yoyote kuharibu amani iliyopo kwa kuwa ni tunu inayowafanya waishi kwa utulivu.

Amewataka kuwakataa watu wanaofika katika maeneo yao kuwashawishi kwa sababu yoyote kuharibu amani na utulivu uliopo.

Mbali na hilo, amewataka wakulima kubadilika kwa kuepuka kuuza mazao yao kwa walanguzi kwa bei ndogo, aweze kupata faida nzuri kupitia vituo vya serikali.

Akizungumza leo Septemba, 25 2024 mkoani Ruvuma leo Rais Dk. Samia amesema uwepo wa amani na utulivu ndio inaifanya Tanzania kuwa salama nawasikubaliane nao kwa sababu maisha wanayoishi Watanzania ni tofauti na nchi nyingine kutokana na amani iliyopo.

“Amani na utulivu ndio inayotufanya majumbani tucheke vizuri, kukiharibika hayo yote hayatakuwepo, niombe sana wale wanaokuja kuwashawishi kwa sababu yoyote ile, kuharibu amani na utulivu katika eneo lenu, msikubaliane nao.

Naomba msikubaliane nao, maisha haya wanayoishi huku kwetu nataka kuwaambia Tanzania ni pepo, pamoja na changamoto zote tulizonazo, Tanzania tupo kwenye pepo ndugu zangu na ukitaka kujua kuwa ni pepo zunguka wala sio mbali kwa majirani utajua kuwa Tanzania upo peponi,” amesema Rais Dk. Samia.

“Nataka kuwaambia kwamba wameishiwa hawana pa kupenya, wameshaona mbele mambo magumu kwao, sasa la kufanya ni kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu ili wananchi waishi kwa mashaka, muone nchi yenu sio njema, ndio lengo lao,” amesema.

Pia amewaomba Watanzania kudumisha amani na utulivu na kuhakikisha kukichagua viongozi bora katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.

“Ni vizuri kutambua kwamba uandiskishaji kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa ni tofauti na uboreshaji wa daftari la wapiga kura, hivyo kama ushaboresha taarifa zako usidhani itakuwezesha kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Niwaombe kuanzia Oktoba 11, mwaka huu jitokezeni kujiandisha ili kupata sifa ya kupiga kura au kugombea katika serikali za mitaa, hili ni muhimu sana, niwaombe wakuu wa wilaya na viongozi wa maeneo haya wa chama na serilali kulizunguymza mara nyingi kwa wananchi,”amesema.

Amewasisitiza viongozi kuendelee kuhubiri umoja na mshikamano katika jamii, wote wanaotaka kuleta fujo kwa kisingizio chochote wawakemee na kuwakataa.

Amesema mkoa wa Ruvuma na nchi ya Tanzania umefikia hatua nzuri kuelekea kupiga hatua za kimaendeleo, wasikubali kurudishwa nyuma kwa siasa zisizojali maslahi na maisha ya wananchi.

Akizungumzia kuhusiana na suala la wakulima, Rais Dk. Samia amewataka wakulima kukubali kubadilika na kufuata manufaa mema ya serikali kwa kuepuka kuuza mazao yao kwa walanguzi kwa bei ndogo ili waweze kupata faida nzuri kupitia vituo vya serikali.

Kauli hiyo aliitoa wilayani Mbiga alipotembelea kituo cha manunuzi ya mahindi cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na kusema serikali imeweka utaratibu wa kununua mazao kwa bei nzuri hivyo wakulima wanapaswa kushirikiana waweze kunufaika.

Amesema ahadi yao ni kuendelea kuondoa shida za wananchi hivyo serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha hali ya wakulima kila inapobaini changamoto hivyo aliwataka wabadilishe mtazamo wao wa masoko.

“Wakulima wenyewe mkubali kubadilika kwa mfano serikali imeweka vituo kadhaa vya kununua mahindi kwa bei kubwa, sasa anapokuja mlanguzi kule kwako kukupa bei ya chini na wewe ukakubali kumpa isilaumiwe serikali.

“Kwa kweli wakulima mbadilike au uongozi wa wilaya muende kwa wakulima mkawafahamishe zile hatua zilizochukuliwa na serikali na kwa nini wasiwape mahindi walanguzi bali wayalete serikalini, naomba muende mkawafahamishe ili wakulima waweze kuuza kwa bei nzuri wapate manufaa kwa jasho lao, warudishe gharama zao kununua pembejeo nyingine,” amesema.

Ameuagiza uongozi wa wilaya kusimamia bei elekezi ya serikali kununua mazao ya wakulima ili muendelee kupata manufaa ya serikali na miradi mingine msiendelee kufanya makosa, kwanza dumisheni amani na utulivu katika wilaya yenu.

Rais Dk. Samia amewasihi wakulima wa mahindi na kahawa kutumia fedha wanazozipata kutokana na mazao hayo kwa uangalifu na kuweka akiba kwa ajili ya maendeleo ya baadaye.

Amewataka wahakikishe wanapanua mashamba yao na kuepuka kutumia vibaya mapato wanayoyapata kutokana na mazao yao.

“Kahawa mnauza bei nzuri sana, niwaombe sana pesa zile tusizichezee ngoma zikaisha.Pesa tuweke akiba kwa mambo ya baadaye , tutanue mashamba zaidi.Leo tumetoa ruzuku lakini huko mbeleni pengine tutasema sasa wakulima jitegemeeni ,” amesema.

Amewasihi kuuza mazao yao kupitia mfumo wa serikali kuhakikisha wanapata bei nzuri na kuepuka kudhulumiwa na walanguzi.

Serikali inakijali kilimo cha kahawa na kuwajali wakulima na imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika kuendeleza kilimo cha kahawa nchini na imeongeza uzalishaji wa mbegu bora za kahawa ambapo kwa mwaka serikali inazalisha miche milioni 20 na kuisambaza kwa wakulima bila malipo.

Pia, imeanza kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa kahawa katika kuhakikisha zao hili linapata soko la uhakika, walianzisha minada ya kahawa ikiwemo njia ya mtandao ili bei ya kahawa iwe ina uhakika, wakulima wauze nje moja kwa moja bila kupita kwa madalali na kupewa bei isiyozingatia maslahi yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post