Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni akipeana mkono na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi(kulia) baada ya kusaini hati ya makubaliano kati ya nchi hizo katika kushirikiana na udhibiti wa matukio ya uhalifu kupitia Jeshi la Polisi na majanga mbalimbali kupitia Jeshi la Zimamoto.Makubaliano hayo yamesainiwa nchini Saudi Arabia.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Ally Senga Gugu akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Serikali ya Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi(kushoto) wakati wa kusaini hati ya makubaliano kati ya nchi hizo katika kushirikiana na udhibiti wa matukio ya uhalifu kupitia Jeshi la Polisi na majanga mbalimbali kupitia Jeshi la Zimamoto.Makubaliano hayo yamesainiwa nchini Saudi Arabia.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni akisaini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Saudi Arabia katika kushirikiana na udhibiti wa matukio ya uhalifu kupitia Jeshi la Polisi na majanga mbalimbali kupitia Jeshi la Zimamoto.Makubaliano hayo yamesainiwa nchini Saudi Arabia.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi(kulia) alisema wakati wa kusaini hati ya makubaliano kati ya nchi hizo katika kushirikiana na udhibiti wa matukio ya uhalifu kupitia Jeshi la Polisi na majanga mbalimbali kupitia Jeshi la Zimamoto.Makubaliano hayo yamesainiwa nchini Saudi Arabia.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu,Riyadh
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati ya makubaliano na Serikali ya Saudi Arabia makubaliano ambayo yanaenda kugusa sekta mbili muhimu za usalama ikiwemo udhibiti wa makosa mbalimbali ya uhalifu kwa kutumia utaalamu na teknolojia ya hali ya juu kwa Jeshi la Polisi sambamba na udhibiti wa majanga mbalimbali ikiwemo moto,ajali za bararani,maporomoko kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Hati hiyo ya makubaliano kwa upande wa Tanzania imesainiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni na upande wa Serikali ya Saudi Arabia imesainiwa na Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi huku pande zote mbili zikionyesha nia ya kubadilishana uzoefu na vifaa mbalimbali ikiwemo vifaa vinavyotumia teknolojia katika udhibiti wa matukio ya uhalifu.
‘Nachukua fursa hii kumshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al -Saudi kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika ziara hii ambayo leo hii imepelekea kukamilisha uwekaji wa saini kwenye hati za makubaliano mbili, moja ikihusisha upande wa Jeshi la Polisi ambapo serikali mbili hizo zinaenda kushirikiana katika kupambana na uhalifu lakini hati ya pili inahusu mashirikiano kwenye Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji na tumezisaini leo hapa na zinakwenda kufungua milango ya kuweza kushirikiana kwa mapana zaidi katika maeneo hayo mawili,hati hii ambayo tumesaini leo itakwenda kufanya sasa nchi yetu kupitia Jeshi la Polisi kuweza kufaidika na fursa mbalimbali za mashirikiano ikiwemo katika kujenga uwezo wa askari wetu katika maeneo mbalimbali na kubadilishana uzoefu na teknolojia na nimefarijika kuona serikali ya Saudi Arabia imeweka msisitizo katika maeneo ambayo hata sisi tumeweka nguvu kuimarisha matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kutoa huduma bora kwa wananchi..’ alisema Waziri Masauni
Waziri Masauni pia aligusia usalama wa kimtandao ambapo alisisitiza uwepo wa kipengele hicho katika hati ya makubaliano ili kuweza kudhibiti uhalifu wa mitandaoni ambao hivi sasa umeanza kushika kasi nchini.
‘Tumeona wenzetu wameweza kuimarika sana katika matumizi ya teknolojia kudhibiti uhalifu wa kimtandao hivyo ni Imani yangu kwamba kupitia mashirikiano ambayo tumesaini kwenye hati ya makubaliano tunakwenda kufanikisha dhamira njema ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuimarisha jeshi letu la polisi katika eneo hilo nak ama mnakumbuka serikali ya awamu ya sita imewekeza fedha nyingi sana kiasi cha dola za kimarekani milioni mia moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa mbali ya vifaa vingine ambavyo tayari vishaingia mwaka huu ambavyo vinahitaji askari wetu wawe na uwezo na uweledi wa kuvitumia sambamba na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao tayari walishaanza kupokea magari.’ Aliongeza Masauni
Akizungumza kwa upande wa Serikali ya Saudi Arabia,Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi alisema wapo tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kudhibiti matukio ya uhalifu huku akigusia uhalifu mbalimbali ulivyodhibitiwa nchini Saudi Arabia ambapo kila mwaka maelfu ya waumini wa dini ya kiislam na wageni kutoka mataifa mbalimbali hufika nchini humo.