Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) umelitaka Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) kumwomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwita muuaji kwani kitendo hicho hakikubaliki.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda amesema umoja huo unawakanya BAVICHA kwa kutoa maneno ya kashifu kwa Rais Samia hali ya kuwa ameimarisha hali ya kisiasa nchini, na kwamba endapo wataendelea na vitendo hivyo watakula nao sahani moja.
“Tunawataka wanawake wa CHADEMA kuomba radhi na kuacha mara moja kukuita wewe muuaji. Tunawakumbusha wasisahau walikualika kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Wanawake wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2023, kwa umuhimu wako walikupatia tuzo ya maridhiano ya kuwa Rais wa kwanza Afrika na duniani kukubali mwaliko kutoka chama cha upinzani,” amesema.
Aidha, Chatanda ameeleza kuwa wote wanaobeza maendeleo yanayofanywa na serikali chini ya Rais Samia Suluhu hawatembei wakaona yaliyofanyika nchini na kumuomba Rais kuachana na maneno ya watu wanaombeza.