WALIOPISHA MAENEO KWA SHUGHULI ZA KISERIKALI MICHESE, DODOMA, KULIPWA FIDIA



Nawandishi wetu, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, ametoa muda wa miezi miwili kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha inakamilisha suala la fidia kwa wananchi wa eneo la Michese Bwawani katika Kata ya Mkonze wanaodai stahiki zao kutokana na kupisha maeneo yao kwa shughuli za Kiserikali.
Hayo yamebainishwa Septemba 04, 2024 wakati wa Mkutano wa hadhara aliouitisha Mkuu wa Mkoa huyo kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi hao uliofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Michese ambapo kero kubwa inayowakabili ni ardhi na malipo ya fidia.

“Mwananchi huyu ameridhia kuipa Serikali ardhi yake kwa manufaa ya umma, lazima sisi tutimize kumpa haki yake ili aweze kutafuta eneo lake mbadala apate nafasi ya kufanya shughuli zake nyingine. Natoa miezi miwili, mpaka mwezi wa 10 mwishoni, wananchi hawa wanaodai fidia za shule na maeneo ya barabara wawe wamelipwa fedha zao” Mhe. Senyamule.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri, amesema licha ya changamoto zinazowakabili wananchi hao, Kata hiyo imepokea fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya elimu na afya.

“Kwa mwaka wa fedha ulioanza, tumepokea shilingi Milioni 191 kwa miradi ya sekta ya elimu na afya kwa maana ya kituo cha afya Mkonze, kujenga uzio kwa Milioni 25 na miradi miwili ya elimu yenye thamani ya shilingi Milioni 166” Amesema Mhe. Shekimweri.

Kadhalika Diwani wa Kata hiyo Bw. David Bochela, ameiomba Wakala wa barabara vijijini (TARURA) kufungua barabara katika eneo hilo kwani idadi ya watu inazidi kuongezeka na barabara inayotegemewa ni moja tu ambapo Mkuu wa Mkoa ameiagiza TARURA kufungua barabara hizo haraka.

Awali, Mhe. Senyamule alitembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika sekta za Afya kwenye Kituo cha Afya Ilazo kinachojengwa na Serikali kwa ufadhili wa UNICEF kikigharimu shilingi Bilioni 3.09, Miradi ya elimu yenye thamani ya jumla ya shilingi Milioni 166.8 ikiwa ni madarasa sita na matundu ya vyoo 16 katika shule za Sekondari za Kata za Itega na Mnadani.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post