NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KATIKA Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zilizofanyika Septemba 11, 2024, wanaharakati wa jinsia walisisitiza umuhimu wa elimu katika kupambana na mila potofu zinazokandamiza haki za wanawake.
Akizungumza katika GDSS, Elizabeth Kiteleko, mwanaharakati kutoka Manzese, alisisitiza kwamba baadhi ya mila potofu bado zinakandamiza haki za wanawake, alitolea mfano mila zinazohusiana na urithi, ambapo mwanamke anapokuwa mjane au yatima, mara nyingi hana haki ya kurithi mali kutoka kwa wazazi au mume.
Aidha Kiteleko alishauri kwamba mila hizi zinahitaji kuboreshwa ili ziendane na wakati wa sasa na kuhakikisha kwamba wanawake wanapata haki zao za msingi kama ilivyo kwa watu wengine.
Kwa upande wake mwanaharakati kutoka Mbagala, Omary Makota alibainisha kwamba mila nyingi bado zinamkandamiza mtoto wa kike, huku akisema kwamba ukosefu wa elimu ndio sababu kuu inayowezesha mila hizi potofu kuendelea.
Pamoja hayo, Makota alitoa wito kwa jamii kuongeza elimu kuhusu haki za wanawake na watoto wa kike ili kuhakikisha kuwa mila hizi zinasahihishwa.
Elimu ni muhimu katika kupinga mila potofu na kuhakikisha usawa wa haki kwa wanawake. Wanaharakati wanakubaliana kuwa kuboresha mitaala ya elimu na kuelimisha jamii ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki za wanawake na watoto wa kike zinaheshimiwa.
Social Plugin